BY RAPHAEL KIBIRITI
Wasomi na wanaharakati wametoa maoni tofauti kufuatia tangazo
lililotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi kuwa,wabunge wake
wanaingia katika Bunge Maalumu la Katiba na ajenda ya kulinda na kutetea
muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Mhadhiri toka katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Mwalimu Bashiru Ally amesema, kimsingi mchakato mzima
kuhusiana na suala hili la kupata katiba mpya ulikosewa toka mwanzo.
“Kwa kuwa muungano wetu ni wa nchi mbili zenye ukubwa tofauti lakini
zilizo na hadhi sawa, tulipaswa kuwa na mjadala wa kitaifa kama
maandalizi, kabla hata ya kuundwa kwa Tume ya Jaji Warioba ili tufikie
maridhiano na maafikiano ya namna ya kuushughulikia mchakato huu,”
alisema.
Alisema endapo hilo lingefanyika, kusingekuwa na haja ya wajumbe wa
kuingia kwenye bunge maalumu kupatikana kwa kuteuliwa kama ilivyokuwa
sasa, bali wangepatikana kwa kupigiwa kura na wananchi, hali ambayo
ingewahakikishia maslahi yao.
Hata hivyo mwalimu Ally aliwaasa wananchi kuondokana na mawazo potofu
kwamba, kitendo cha CCM kuwa na wajumbe wengi kwenye bunge maalumu la
katiba, ni tiketi ya kupata katiba mbaya.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Deus Kibamba alitofautiana na
msimamo huo wa CCM, akisema kitendo hicho cha kutoa maelekezo kwa
wabunge wake wachukue msimamo fulani wa kichama ni cha kulivuruga bunge
maalumu kabla hata halijaanza.
Comments