WANAWAKE
na maendeleo, tufanye kazi, tusonge mbele, yelele…yelele… Hii sehemu ya
mashairi ya wimbo wa staa wa muziki wa kizazi kipya na Mbunge wa Viti
Maalum (UVCCM), Geita, Vicky Kamata anayetajwa kuwa na utajiri balaa.
UWAZI LINA KILA KITU
Vicky amepata mafanikio makubwa ambayo kila mwanamke Tanzania angependa
kuyapata. Gazeti hili lilimchimba kwa kina na kupata utajiri wote
alionao kwa sasa.
KABLA YA SIASA, KABLA YA BONGO FLEVA
Kabla ya siasa aliishi maisha ya dhiki ambayo hakutegemea kama angekuja
kupata mafanikio makubwa. Ni miongoni mwa Watanzania waliozaliwa katika
familia duni. Katika kutafuta ‘kutoka’ kimaisha, Vicky amewahi kuwa
mwanamuziki wa Bongo Fleva na kutunga nyimbo mbalimbali, wimbo wa
Wanawake na Maendeleo ndiyo uliomtambulisha zaidi katika jamii.
“Nimezaliwa
kwenye familia duni, nimeishi maisha ya dhiki sana, mbali na muziki,
nimewahi kuwa mwalimu wa shule ya msingi kule Moshi (Kilimanjaro) katika
harakati za kusaka maisha, baadaye nilikwenda Morogoro.
“Kila kitu
kinabadilika kama ukimwamini Mungu,” alisema Vicky mwenye watoto wawili,
Revocatus na Glory (jina la baba halikutajwa).
MAFANIKIO YAANZA
Mwaka 2006, Vicky alifanikiwa kuajiriwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
akiwa ni afisa uhusiano. Mwaka 2010, Vicky alifanikiwa kuwa mbunge wa
viti maalum akiuwakilisha Mkoa wa Geita.
MJENGO WA GHOROFA MBILI
Akiwa mbunge, Mheshimiwa Vicky ameingia kwenye orodha ya wanawake
mabilionea nchini kwa kuangusha mjengo wa kifahari wa ghorofa mbili
Sinza jijini Dar es Salaam wenye thamani ya shilingi bilioni moja na
milioni mia nne. Ndani ya ghorofa hilo kuna bwawa la kisasa la kuogelea
‘swimming pool’ ambalo linatumiwa na familia yake.
MAGARI YAKE SASA
Kama walivyo matajiri wengine, mheshimiwa huyo anamiliki magari manne ya
kifahari, yote yakiwa na thamani ya shilingi milioni 261. Ana Toyota
Voxy- Noah ambalo alilitoa sokoni kwa shilingi milioni 16. Kamata pia
anamiliki BMW X5 likiwa na thamani ya shilingi milioni 130. Mara nyingi
anapokwenda bungeni, Vicky hutembelea gari linalomudu mikiki ya
barabarani, Toyota Land Cruiser ‘VX’ ambalo lina thamani ya shilingi
milioni 90. Pia mwanamama huyo ana gari aina ya Toyota Altezza
alilolinunua kwa shilingi milioni 25.
ANAMILIKI MGODI WA DHAHABU
Wakati hayo yakiwa wazi, chanzo makini kilidai kuwa, mheshimiwa huyo
amenunua mgodi wa dhahabu Geita, jambo ambalo ni sehemu kubwa ya
mafanikio yake. “Vicky amenunua mgodi wa dhahabu Geita, mimi ni mtu
wangu wa karibu, hapendi kusema mafanikio yake wala watu wajue lakini
ukweli ndiyo huo. Eneo ni kubwa, muda si mrefu uchimbaji utaanza,”
kilisema chanzo cha habari kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
ANA SHAMBA LA EKARI 157
Utajiri wa mheshimiwa huyo unaendelea kuanikwa kuwa, ni pamoja na
shamba lenye ekari 150, Kisarawe, Mkoa wa Pwani. Pia ana shamba la miti
Kibamba, Dar lenye ekari 7.
NI MFUGAJI
Mbali na mambo mengine, Vicky ni mfugaji kama ilivyo asili ya Wasukuma. Anafuga ndege aina ya kanga, kuku wa kisasa na mbuzi.
ANASOMESHA WATOTO WASIOJIWEZA
Katika mambo ambayo huenda yanachangia kuchota baraka, mheshimiwa Vicky
anawalipia ada ya sekondari watoto yatima, walemavu na wasiojiweza
kimaisha, idadi yao ikifikia 75.
KIPATO CHAKE KIKOJE?
Dodoso zinaonesha kwamba, kwa kazi ya uheshimiwa, kwa mwezi anaingiza
shilingi milioni 15 ukijumlisha posho zote za ubunge, ujumbe wa kamati
ya bunge na mshahara.
AMFUNIKA ANNE MAKINDA
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, jumba la kifahari la
Vicky Kamata linalifunika lile la bosi wake ambaye ni spika wa bunge,
mheshimiwa Anne Makinda. Yeye nyumba yake ipo Kijitonyama.
ULINZI NYUMBANI KWAKE USIPIME
Uwazi lilipata bahati ya kufika nyumbani kwa Vicky na kukumbana na
ulinzi wa mitambo ya kisasa ya kuzuia wezi na majambazi kwa saa 24. Ili
mgeni aingie ndani ya geti huhojiwa na walinzi kwa dakika zisizopungua
kumi.
WABAYA WAKE WAMUUNDIA ZENGWE LA FREEMASON
Huwezi kupendwa na kila mtu, hii ni baada ya mwandishi wa gazeti hili
kuamua kupiga kambi kwa muda wa siku mbili jirani na nyumba ya
mheshimiwa huyo ambapo baadhi ya watu waliohojiwa kuhusu ukwasi wa
mbunge huyo mwanamke walisema huenda ni memba wa Freemason. “Mafanikio
ya mbunge huyu bwana ni makubwa mno, tunasikia watu wakisema huenda ni
Freemason. Lakini ndivyo tulivyo Watanzania, mtu akifanikiwa kidogo
wanasema ni Freemason, ninavyomfahamu huyu dada amepiga hatua, sijawahi
kumsikia na mambo ya Freemason,” alisema jirani mmoja na kuungwa mkono
na wenzake.
MSIKILIZE VICKY
Katika mahojiano maalum na Uwazi kuhusu utajiri wake, Vicky alisema:
“Mafanikio yote yametokana na juhudi zangu za kujituma katika kufanya
kazi, namwamini Mungu siku zote. Hakuna dhambi mbaya hapa duniani kama
kukata tamaa. “Tukifanya kazi kwa kujituma na kumwamini Mungu hakuna
Mtanzania maskini. “Kila mtu ana uwezo wa kubadilisha mfumo wa maisha
akiamua, umaskini wa watu si chaguo la Mungu, kila jambo litokealo kwa
mwanadamu lina maana kubwa kwa Mungu.”
KAULI YA UWAZI
Wanawake nchini waige mfano wa Vicky kwa kukamata fursa mbalimbali na
wanapofanikiwa wawasaidie wengine, kama kusomesha yatima na
wasiojiweza.
Kwa hisani ya GPL
Comments