Dar es Salaam. Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete hatakubali kuidhinisha
kama akipelekewa ombi la kuongeza kiinua mgongo cha wabunge kutoka Sh43
milioni hadi Sh160 milioni.
Wabunge wakimsikiliza Rais Jakaya Kikwete
alipokuwa akiwahutubia kwenye Ukumbi wa Bunge, mjini Dodoma, Novemba 7
mwaka jana. Picha ya Maktaba
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema jana kuwa Rais
Kikwete hajapokea maombi hayo huku akipinga maelezo kuwa Serikali
ilishayakubali.
Gazeti dada la The Citizen wiki iliyopita, lilimkariri Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya akisema Serikali ilikuwa imepitisha kupandishwa kwa kiwango
cha kiinua mgongo kutoka Sh43 milioni hadi Sh160 milioni baada ya
kumaliza kipindi cha miaka mitano.
Waziri huyo alikaririwa akisema kuwa kiwango hicho kilipitishwa na Ofisi
ya Waziri Mkuu na tayari wabunge walishaanza kuchukua fedha hiyo licha
ya ukweli kuwa Bunge hili halijamaliza muda wake.
Hata hivyo, Rweyemamu alisema nao wamelisoma suala hilo kwenye magazeti
na kwamba halijafika Ofisi ya Rais... “Suala hili halijafika Ofisi ya
Rais hata kama litaletwa, `I really doubt if the President will endorse
such matter’ (Nina shaka kama Rais ataidhinisha suala hili).”
Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi tayari imekanusha vikali taarifa za
kupandishwa kiwango hicho cha malipo kwa wabunge.
Comments