Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika Au, Addis Ababa nchini Ethiopia |
Na Flora Martin Mwano
Viongozi wa nchi za Afrika wamekubaliana kuendelea kuchukua hatua zaidi
kudhibiti machafuko yanayozikumba nchi wanachama sambamba na kuunda
kikosi cha dharura kitakachoshughulikia migogoro inayolikumba bara hilo,
azimio hilo limefikiwa jana katika siku ya mwisho ya mkutano wa
viongozi wa Umoja wa Afrika AU mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Viongozi walioshiriki mkutano huo wa siku mbili wametaka kuchukuliwa kwa
hatua za haraka ili kuikoa nchi ya Sudani Kusini na Jamhuri ya Afrika
ya Kati ambazo zinakumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti mpya wa AU ambaye ni Rais wa
Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz amesema nchi wanachama zitatoa
wanajeshi watakaounda kikosi hicho.
Mkuu wa Kamisheni ya AU, Nkosazana Dlamini Zuma amethibitisha kuwa
tayari mataifa nane yameahidi kutoa wanajeshi wake katika kikosi hicho
ambacho mchakato wake ulijadiliwa pia katika mkutano wa mwaka jana wa
umoja huo.
Nchi zilizoahidi kutoa wanajeshi wake ni Algeria, Angola, Chad, Ethiopia, Guinea, Mauritania, Afrika Kusini, Tanzania na Uganda.
Chanzo: kiswahili.rfi.fr
Comments