Mashindano ya Vyuo vikuu ya Zain Afrika Challenge (ZAC) yanaendelea tena hapo kesho kwa kuvikutanisha vyuo vikuu vya Africa Nazarene kutoka Kenya na Chuo Kikuu cha Njala kutoka Sierra Leone.
Hili litakuwa ni shindano la tatu tangu mashindano hayo yaanze kwa mwaka huu. Katika mashindano ya awali Chuo kikuu cha Makerere kiliwabwaga Chuo kikuu cha Malawi wakati Chuo kikuu cha Arusha kilishindwa kufurukuta dhidi ya Chuo Kikuu cha Ghana.
Vyuo Vikuu 16 vitachuana kuwania kitita cha dola za Marekani USD 50,000 pamoja na Kombe la Zain, ambayo ndiyo zawadi ya mabingwa. Wanafunzi wa chuo kitakachoshinda watakaoshiriki katika mtoano huo kila mmoja wao atandoka na dola za Mareka USD 5000.
Kwa mwaka huu Tanzania inawakilishwa na Vyuo Vikuu viwili ambavyo ni Chuo Kikuu cha Tumaini pamoja na Chuo Kikuu cha Arusha.
Hata hivyo Arusha tayari wamekwishatolewa, na kuwafanya watanzania sasa kuomba dua ya ushindi kwa Chuo kikuu cha Tumaini.
Wateja wa mitandao yote nchini safari hii wataweza kujibu maswawali yanayoulizwa wakati na mtoani na kujishindia zawadi nono ambazo ni pamoja na simu mpya za mkononi aina ya Nokia N97 zenye thamani ya zaidi ya shilingi laki nane. Kushiriki katika mchezo wa ZAC watu wenye simu za mkononi watatuma majibu ya swali litakaloulizwa kwenda 15315. Zawadi hizi zitatolewa kila wiki ambapo watachaguliwa washindi watatu kila wiki.
Timu 100 kutoka Vyuo Vikuu vinavyoongoza kutoka nchi nane za Afrika ambazo ni; Tanzania, Ghana, Kenya, Malawi, Nigeria, Sierra Leone, Uganda na Zambia zilichuana katika mashindano ya awali ya kitaifa ili kutafuta nafasi ya kuwakilisha nchi zao katika mtoano wa kimataifa na kujipatia fursa ya kujishindia sehemu ya zawadi zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja (Dola za Marekani 1,000,000).
Kati ya timu hizo 100, timu 32 zilizoongoza zimefuzu kushiriki katika mashindano ya kimataifa yanayofanyika nchini Uganda katika ushindani wa hali ya juu ili kuwania nafasi ya kushiriki fainali ya mashindano ambayo yatarushwa na luninga katika nchi zote nane zinazoshiriki na pia kwa mara ya kwanza, mashindano haya yatarushwa Afrika nzima kupitia satellite ya DSTV na yatatazamwa na zaidi ya watu milioni 700 kila Jumatatu saa moja na nusu usiku kuanzia Machi 1, 2010 kwenye kituo cha Africa Magic.
Chuo Kikuu cha Makerere cha Uganda kitakuwa chuo kikuu cha kwanza kushiriki katika mashindano hayo yatakayo rushwa kwa muda wa wiki 16 kikichuana na Chuo Kikuu cha Malawi.
Katika msimu wa tatu wa Zain Africa Challenge uliofanyika mwaka jana Chuo Kikuu cha Ibadan cha Nigeria kiliibua na ushindi katika mtoano huo wa chemsha bongo na kujinyakulia zaidi ya milioni 60 (USD 50, 000) kutoka Zain, wakati kila mshiriki alijipatia kitita cha dola za Marekani 5000 kila mmoja.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Chuo Kikuu cha Kenyatta ambacho kiliondoka na dola za Marekani 35,000, na kila mshiriki dola 3,500. Vyuo vingine vyote vilivyoshiriki vilipata zawadi zenye thamani kati ya dola 5000 na dola 25,000.
Maswali katika mtoano wa ZAC yanagusa maeneo mbali mbali ikiwemo, historia, sayansi, utamaduni wa Africa, Jiographia, literature, muziki ya matukio ya wakati huo. Kadhalika ZAC huonyesha fursa zilizopo za kielemu katika Vyuo Vikuu vya Afrika kupitia video na wasifu wa wanafunzi
Comments