Dodoma. Saa chache baada ya Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2013/14
kutupwa na Bunge jana, wabunge wa CCM wameshikana uchawi huku wakitaka
kuwatosa wenzao wanaowatuhumu kusababisha kadhia hiyo.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe (wa pili kushoto), Naibu Waziri
wa Maji, Dk Binilith Mahenge (kushoto) na Mbunge wa Musoma Mjini
(Chadema), Vicent Nyerere baada kuahirishwa kwa kikao cha Bunge, Dodoma
jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Wabunge wa CCM walikutana katika kikao cha dharura kilichoongozwa na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kujadili hatua ya Bunge kukataa bajeti hiyo
kwa maelezo kwamba haina suluhisho la kuwaondolea wananchi matatizo ya
maji.
Kelele za wabunge wa CCM na wale wa upinzani zilimlazimisha Spika wa
Bunge, Anne Makinda kuiondoa bungeni na kuitaka Serikali ikajipange upya
na kuiwasilisha Jumatatu.
Baada ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge jana mchana, wabunge wa CCM
walikutana na habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema wabunge Kangi
Lugola (Mwibara) na Deo Filikunjombe (Ludewa) walishambuliwa kutokana na
kile kilichodaiwa kwamba wamekuwa wakiidhalilisha Serikali ya CCM
bungeni.
Habari zinadai kwamba waliowashambulia wabunge hao ni wenzao, Saidi
Nkumba (Sikonge) na Livingstone Lusinde (Mtera) ambao kwa nyakati
tofauti walitamka kwamba hawaisaidii Serikali na kwamba bora wakahamia
upinzani kuliko kuendelea kukichafua chama hicho.
Comments