KLABU ya Yanga inatarajia kuandaa hafla ya kuchangisha michango kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wake mpya wa kisasa maeneo ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa, mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa habari hizo, uamuzi wa kuandaa hafla hiyo ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo kilichofanyika hivi karibuni mjini Dar es Salaam.
"Kamati ya utendaji iliyokutana hivi karibuni ilikubaliana kuandaa hafla kubwa ya kuchangisha mamilioni ya pesa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo,"alisema mmoja wa viongozi wa kamati hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mbali ya kuandaa hafla hiyo, kamati hiyo imeshapendekeza ramani ya uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 40,000, ambao ujenzi wake unatarajiwa kugharimu dola milioni 50 za Marekani
Chanzo hicho cha habari kilieleza kuwa, uwanja huo ndio chaguo la kwanza katika ramani zilizochorwa na kuwasilishwa kwa uongozi wa Yanga na Kampuni ya Beijing Construction Engineering tawi la Tanzania.
Kiliongeza kuwa, chaguo la pili ni uwanja ambao ujenzi wake utagharimu dola milioni 40 na wa tatu ujenzi wake utagharimu dola milioni 30.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema, anachojua ni kwamba mchakato wa ujenzi wa uwanja huo bado unaendelea.
"Mambo yatakakapokamilika, uongozi utaweka wazi kila kitu kwani muda si mrefu, ndoto ya klabu yetu kumiliki uwanja wa kisasa itakamilika,"alisema.
Mwezi uliopita, Kampuni ya Beijing Construction Engineering tawi la Tanzania, kupitia Meneja Msaidizi wake, Zhang Chengwei alisema, ujenzi wa uwanja huo utaanza mara baada ya uongozi wa Yanga kupata fedha.
Chengwei alisema uwanja huo utakuwa na sehemu ya maduka, hoteli, migahawa, 'super market', sehemu ya maegesho ya magari na uwanja mdogo wa mazoezi.
Alisema iwapo Yanga itakuwa na fedha za kutosha, watajenga uwanja huo kwa kipindi cha mwaka mmoja na utafanana na uwanja uliojengwa na kampuni hiyo nchini Afrika Kusini.
Kampuni hiyo ndiyo iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Uwanja wa Uhuru, jengo la maonyesho la Chuo Kikuu cha Elimu (DUCE), uwanja wa ndege wa Zanzibar, jengo la mapumziko la wageni mashuhuri katika uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere na ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).Inatoka kwa mdau.
Comments