Korea Kaskazini nayo inajiandaa kukabiliana na vita hivyo hatari vinavyotarajiwa kuanza muda wowote
Magari ya kivita yakiwa yameegeshwa katika
mji wa Panju nchini Korea ya Kaskazini tayari kabisa kwa mashambulizi
yanayotarajiwa kufanywa na Korea Kusini inayosaidiwa na Marekani.Picha
na AFP
Washington. Marekani imepeleka ndege za kivita Korea Kusini kwa lengo la
kusisitiza dhamira yake ya kuisaidia nchi hiyo.Imedaiwa kwamba msaada
huo unaotolewa na Marekani kwa nchi hiyo ni msaada wa kijeshi dhidi ya
vitisho vya Korea Kaskazini.
Ndege hizo aina ya F-22 zinadaiwa kupelekwa kwenye ngome ya kikosi cha
anga huko Osan, ngome kuu ya kikosi cha anga cha Marekani nchini Korea
Kusini. Hata hivyo, Marekani haijasema ilipeleka ndege ngapi za kivita
Korea Kusini kutoka kwenye ngome yake ya kikosi cha anga cha Okinawa,
Japan.
Wasiwasi uliongezeka tangu kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un
kuamuru jaribio la silaha za nyuklia mwezi Februari, mwaka huu.
Wiki iliyopita Korea Kaskazini ilisema kuwa inaingia katika vita na
Korea Kusini, katika mwendelezo wa vita vya maneno dhidi ya utawala
mjini Seoul na Washington.
Hii ni baada ya kuwekewa vikwazo vya kimataifa kufuatia jaribio lake la
silaha za nyuklia.Shirika la Habari la Korea Kaskazini KCNA, lilitoa
taarifa inayosema kuwa kuanzia sasa, uhusiano wa Kaskazini na Kusini
utaingia katika hali ya vita, na kwamba masuala yote yanayojitokeza kati
ya pande hizo yatashughulikiwa ipasavyo.
Comments