Na Victor Melkizedeck Abuso
Polisi mjini Boston nchini Marekani wanasema kuwa mmoja wa washukiwa
waliotekeleza mashambulizi ya bomu wakati wa mashindano ya riadha siku
ya Jumatatu na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine 170
kujeruhiwa ameuawa kwa kupigwa risasi.
Hata hivyo, polisi wanasisitiza kuwa mshukiwa mwingine bado anasakwa baada ya kukabiliana na polisi kwa kufwatuliana risasi.
Mshukiwa huyo amepoteza maisha akiwa kizuizini baada ya kupigwa risasi na badaye kuzuiliwa mjini Boston.
Awali, maafisa wa Ujasusi wa FBI nchini Marekani walitoa picha za
washukiwa wawili wanaotuhumiwa kutekeleza mashambulizi hayo wawili .
Picha za washukiwa hao zilitolewa kupitia kanda za usalama za CCTV
zikionesha wanaume wawili wakiwa wamevaa nguo nyeusi, kofia za mchezo wa
baseball na wakiwa na mifuko migongoni.
Richard DesLauriers mmoja wa maafisa wa FBI amesema kuwa washukiwa hao
ni hatari sana na wananchi wa Marekani hawastahili kuwakaribia.
Mepema juma hili, FBI ilitoa picha za kifaa cha jikoni kilichotumiwa
kutekeleza mashambulizi hayo pamoja na washukiwa hao wakitupa mifuko yao
katika eneo la kumalizia mbio hizo ndefu.
Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu watatu na kuwajeruhi
wengine 170 wakiwemo watoto watatu ambao madaktari wanasema hali yao
bado haijatengemaa.
Comments