Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amekanusha malalamiko kwamba wananchi hawakuelezewa ipasavyo kuhusu katiba mpya.
Bwana Mugabe aliiambia BBC kwamba Wazimbabwe walishauriwa sana kuhusu katiba hiyo na walitoa maoni yao.
Kura ya maoni kuhusu katiba mpya inafanywa nchini Zimbabwe leo.
Chama cha Rais Mugabe cha Zanu-PF na kile cha
MDC cha Morgan Tsvangirai ambacho kimo kwenye serikali ya mseto,
vinaunga mkono katiba mpya.
Waandishi wa habari wanasema wakati wa kampeni
pamekuwa na mvutano nchini Zimbabwe kabla ya uchaguzi mkuu ambao
unatarajiwa kufanywa baadae mwaka huu.
Vyama vikuu vya Zimbabwe vina msimamo mmoja kuhusu katiba inayopendekezwa.
Vinaiunga mkono.
Inavoelekea katiba itakubaliwa na wengi lakini inawezekana wataojitokeza kupiga kura ya maoni ni wachache.
Katiba hiyo ni muhimu kuielekeza nchi kwenye uchaguzi huru na wa haki.
Ina vipengee vya haki za wananchi na vizuizi dhidi ya madaraka ya rais mtendaji.
La kutatanisha ni kuwa katiba mpya inataka rais
atumike kwa mihula miwili ambayo itampa Rais Mugabe, mwenye umri wa
miaka 89, uwezekano wa kuongoza kwa miaka kumi zaidi.
Comments