Muungano cha CORD nchini Kenya umetaka zoezi la kuhisabu kura za uraisi
nchini humo lsitishwe na kuelezea wasiwasi wake juu ya uadilifu wa zoezi
ambalo siku tatu baada ya upigaji kura limeshindwa kukamilika.
Kauli hii inatajwa kwamba inaweza kuutia kasoro kubwa uchaguzi wa hapo
Jumatatu (tarehe 4 Machi), ambao hadi sasa umetajwa na waangalizi wa
kimataifa kwamba ulikuwa wa amani na wa wazi.
Mgombea wa CORD, Waziri Mkuu Raila Odinga, yuko nyuma ya mgombea wa
muungano wa Jubilee, Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta, wakati kura
zikiendelea kuhesabiwa.
Hata hivyo, mgombea mwenza wa Odinga, Kalonzo Musyoka (pichani juu),
amesema kauli ya muungano huo haipasi kuchukuliwa kama wito wa umma
kuchukua hatua na amewataka wapiga kura kuendelea kuwa watulivu na
wastahmilivu.
Ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 nchini humo, zilipelekea
kiasi cha watu 1,200 kuuawa na zaidi ya 600,000 kulazimika kuyahama
makaazi yao.
"Sisi kama muungano wa CORD tunaamini kwamba zoezi hili la kuhisabu kura
limekosa uhalali na lazima lisimamishwe na liazishwe upya kwa kutumia
fomu kutoka vituo vya kupiga kura," Musyoka aliwaambia waandishi wa
habari.
Comments