MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ambao ni
wachapishaji wa magazeti ya Rai, Mtanzania, Dimba na Bingwa, Absalom
Kibanda, amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana
nyumbani kwake kisha kupigwa na kujeruhiwa vibaya.
Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
alipigwa na kitu kizito chenye ncha kali kichwani, kutobolewa jicho la
kushoto, kung’olewa ukucha wa kidole cha mkono na meno.
Tukio hilo linakuja ikiwa ni miezi takriban tisa tangu kutekwa, kuteswa,
kuumizwa vibaya, kung’olewa meno na kucha na kisha kutelekezwa msituni
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, usiku
wa Juni 26, mwaka jana.
Tangu kutokea kwa tukio la Dk. Ulimboka ambalo linafanana kabisa na hili
la Kibanda, Jeshi la Polisi nchini limekuwa likitupiana mpira katika
kueleza hatua zilizofikiwa kuwasaka watuhumiwa waliohusika.
Pamoja na mtuhumiwa mmoja anayedaiwa kuwa raia wa Kenya, Joshua Mulundi,
kufikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika na tukio hilo, bado Jeshi la
Polisi halijawahi kumhoji Dk. Ulimboka wala watuhumiwa aliowataja kwa
majina kuwa walihusika kumteka na kumtesa.
Katika tukio la Kibanda, inaelezwa kuwa watuhumiwa hao ambao
hawajakamatwa walimtendea unyama huo akiwa nyumbani kwake eneo la Mbezi
Beach usiku wa saa sita akiwa ndani ya gari akingojea kufunguliwa lango.
Tukio hili pia limetokea wakati Kibanda akikabiliwa na kesi ya uchochezi
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo anashitakiwa na Jamhuri
akidaiwa kuchapisha makala katika gazeti la Tanzania Daima ambalo
alikuwa Mhariri Mtendaji wake.
Kesi hiyo ambayo ilikuwa imepangwa kuendelea kusikilizwa jana,
iliahirishwa baada ya mawakili wake kuwasilisha ombi mahakamani kueleza
tatizo alilolipata mteja wao.
Comments