Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud Reuters/Tiksa Negeri |
Na Flora Martin Mwano
Baraza la usalama la umoja wa Mataifa UNSC limeondoa vikwazo vya
biashara ya silaha dhidi ya Taifa la Somalia kwa kipindi cha mwaka mmoja
ili kuweza kuisaidia Serikali ya Somalia katika kupambana na Wanamgambo
wa Kiisalmu wanaokabiliana na serikali hiyo.
Nchi wanachama 15 wa Baraza la usalama kwa pamoja walipitisha azimio la
kuruhusu silaha nyepesi kuuzwa kwa vikosi vya kijeshi nchini Somalia
wakati huu ambapo wanapambana kuilinda Mamlaka ya Somalia dhidi ya kundi
la wanamgambo la al Shabaab lenye uhusiano mtandao wa kigaidi duniani
wa Al Qaeda.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mahmoud aliyechukua madaraka ya nchi hiyo
mwezi Septemba mwaka jana amekuwa akishinikiza Baraza la Usalama kuondoa
vikwazo vya biashara ya Silaha kwa nchi hiyo.
Mohamud amepokea kwa mikono miwili hatua ya umoja wa Mataifa akisema
kuwa inaashiria kuimarika kwa hali ya kisiasa nchini Somalia na
kutasaidia wanajeshi wake ambao mara kadhaa wamekuwa wakikabiliwa na
uhaba wa silaha pale wanapopambana wa wapiganaji wa Al Shabaab.
Source: kiswahili.rfi.fr
Comments