Na Deodatus Balile, Dar es Salaam
Viongozi wa dini nchini Tanzania wamelaani wimbi lililoibuka hivi
karibuni la machafuko yanayotokana na tofauti za kiimani kati ya
Wakristo na Waislamu ambayo tayari yameshasababisha vifo vya viongozi
watatu katika kipindi cha mwezi Februari, na kuapa kuzirejesha jamii
hizi mbili katika hali ya kawaida.
Baadhi za viongozi hao wanasema kuwa
mahubiri yanayotelewa bila kuwa na kibali husika kwenye makanisa na
misikiti ndio kiini cha hali ya mtafaruku inayoendelea sasa. Juu,
wanaume wakifanya ibada msikitini jijini Dar es Salaam. [Na Mwanzo
Millinga/AFP]
Tarehe 11 Februari, mzozo kati ya wafuasi wa dini hizo mbili juu ya nani
anafaa kuchinja nyama ulisababisha kifo cha mchungaji Mathayo Machila
aliyekuwa na umri wa miaka 45 na kusababisha wananchi wengine
kujeruhiwa. Tangu wakati huo serikali imeanzisha kamati ya viongozi wa
dini kwa lengo la kurejerea sheria za kiimani kuhusu kuchinja mifugo
mbalimbali kwa ajili ya nyama.
Visiwani Zanzibar, Mchungaji Evarist Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi na
watu wasiojulikana nje ya kanisa lake tarehe 17 Februari, wakati pia
tarehe 23 Februari Sheikh Ali Khamis Ali, 65, aliuawa na watu
wasiojulikana kwenye shamba lake la minazi.
Mauwaji hayo ya mwezi Februari ni mwendelezo wa matukio yaliyoanza mwaka
uliopita. Katika sherehe za Krismasi, watu waliokuwa na silaha
walimshambulia kwa risasi Mchungaji Ambrose Mkenda wakati alipokuwa
njiani akirejea nyumbani, na mwezi Novemba watu wasiojulikana
walimshambulia kwa kumwagia tindikali Sheikh Fadhil Soraga.
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, amesema kuwa nchi inatakiwa kuhamasisha uvumilivu wa kidini.
"Tumekuwa tukivumiliana kwa muda mrefu lakini sasa uvumilivu huo
umekwenda wapi?" aliiambia Sabahi. "Serikali, viongozi wa dini na
wanasiasa wanapaswa kuhubiri amani, upendo na utulivu."
Comments