Na Hellen Ngoromera
WANAFUNZI 5,157 wa sekondari wamefukuzwa shule mwaka 2011 kutokana na kugundulika kupata ujauzito.
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na mratibu wa mafunzo ya
jinsia kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Winifrida
Rutaindurwa katika semina ya waandishi wa habari kuhusu changamoto
zinazowakabili watoto wa kike.
Akizungumza katika semina hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), alisema idadi hiyo ambayo ni sawa
na asilimia 6.8 ni ndogo ikilinganishwa na ya waliobainika kupata
ujauzito na kufukuzwa mwaka 2010 ambao walikuwa 5,346 sawa na asilimia
8.1.
Kwa mujibu wa mtaribu huyo, katika utafiti wao wamebaini kwamba vyanzo
vikuu vya tatizo hilo ni ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa wanafunzi hao
hali inayowafanya wengi wao hasa wanaosoma mijini kushawishika na
lifti.
Vyanzo vingine ni umbali wa shule na maeneo wanayoishi, ukosefu wa
mabweni kwa wanaosoma shule za kutwa na nyingine, matumizi mabaya ya
teknolojia ikiwemo televisheni, mitandao ya kijamii kama face book,
twiter na vingine.
Alisema ili kuepuka matatizo hayo, ni vyema jamii ikatambua kwamba
watoto wa kike pia wanapaswa kupewa fursa kama walivyo watoto wa kiume
hasa katika masomo.
Chanzo: Tanzania Daima
Comments