Na Anna Nkinda – Magu
Kina mama Wajasiliamali nchini wametakiwa kuongeza ubunifu katika
vikundi vyao ikiwa ni pamoja na kutengeneza bidhaa bora zaidi ambazo
zitakidhi kiwango cha kimataifa na hivyo kuwa na soko la uhakika la
ndani na nje ya nchi.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
wakati akiongea na wanawake wajasiliamali wa mkoa wa Mwanza kwenye
kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke Duniani zilizofanyika katika
kituo cha utamaduni Bujora wilayani Magu.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) pia aliwataka wanawake hao wajasiriamali kutengeneza
mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kutafuta masoko ya bidhaa zao hasa
mayai na vyakula ambayo yanapatikana kirahisi katika mkoa wa Mwanza na
mikoa jirani.
Aliendelea kusema kuwa hivi sasa kina mama wengi wanaungana na kufanya
kazi kwa pamoja katika vikundi vya ujasiriamali hii ni ishara kuwa kila
mwanamke anashauku ya kufanya kazi ya maendeleo bila ya kutegemea
msaada wa mwanaume.
Mama Kikwete alisema, “Ninawashukuru kwa kazi njema mnazozifanya na
ninapenda kuwahakikishia kuwa niko nanyi katika mihangaiko na juhudii
zenu zote. Nitajitahidi niwezavyo na kadri Mungu atakavyonijalia
kuwawezesha katika elimu ya ujasiriamali kupitia taasisi ya WAMA kila
itakapowezekana”.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisisitiza kuwa juhudi za ukombozi wa mwanamke
zilianza zamani na mtu mmojammoja. Lakini kwa sasa juhudi hizi zinapaswa
kuenziwa kwa mshikamo na kuwa wamoja zaidi ili kila mtu kwa nafasi
yake aweze kumkomboa mwanamke kielimu na kiuchumi.
Comments