Neno La Leo; Na Tuyaishi Maisha Ya Kadiri...
Ndugu zangu,
DUNIANI hakuna miujiza katika kuyafikia mafanikio. Hakuna njia za mkato pia. Ni sharti tufanye kazi kwa bidii. Tusiwe ni watu wenye kutanguliza taamaa na hata kuwadhulumu wengine. Tuyaishi maisha ya kadiri. Ni kwa kuyafanya yale yaliyo ndani ya uwezo wetu. Si kuishi kwa kufikiri wengine wanavyotaka uishi.
Maana, ni wachache duniani walioweza kufanya miujiza kama tunayoambiwa kwenye vitabu vya dini; Bwana Yesu yu miongoni mwa wachache hao. Tunasoma, kuwa Mafalisayo walimshangaa Yesu na mafanikio yake. Wakatamka; “ Hivi ni Yesu huyu huyu mwana wa Joseph fundi Seremala!”
Naam, mwanadamu usitazame tu alipofikia sasa mwanadamu mwenzako kwenye safari yake. Jitahidi uangalie mwanzo wa safari yake. Alikotokea. Ndipo hapo utayapata ya kujifunza.
Papa Francis wa Kanisa Katoliki amefikia kiwango cha juu cha mafanikio kwenye ngazi ya kanisa. Ni rahisi kumwangalia hapo alipo, lakini ni muhimu kuiangalia safari yake ilipoanzia.
Tunasoma leo, kuwa Papa Francis ni mtu wa kadiri. Muda wote wa uhai wake amejitahidi kuishi maisha ya kadiri. Papa si mtu wa makuu. Na kule Vatican wanashangazwa hata na mavazi yake yasio gharama kubwa, ikiwamo viatu pia.
Hapa kwetu Tanzania Julius Nyerere ni mfano wa viongozi walioishi maisha ya kadiri. Mwalimu aliishi kama alivyohubiri. Ni mfano wa kuigwa.
Ni Neno La Leo
Maggid Mjengwa,
Iringa
Comments