KIUNGO Erasto Nyoni wa timu ya ‘wauza koni’ wa Azam FC, amesema kanuni iliyorejeshwa msimu huu na Shirikisho la Soka, TFF, ya kuzitaka klabu za ligi kuu ya Bara kutosajili wachezaji wa kigeni zaidi ya watano ni nzuri kwani itasaidia ligi hiyo kuwa na wageni ngangari.
Nyoni aliyewahi pia kuwa mchezaji wa kigeni katika ligi kuu ya Burundi wakati akikipiga katika klabu ya Vital ‘O ya Bujumbura msimu wa 2006, aliiambia Lete RAHA jana Jumamosi kuwa, kurejeshwa kwa kanuni hiyo kutazilazimisha timu zote kusajili ‘vifaa’ vya ukweli, na si kupapatikia majina makubwa ya wageni ‘waliofulia’ na wasio na kiwango bora uwanjani.
"Mimi naamini uamuzi wa kutumiwa kwa kanuni hii una faida nyingi kuliko hasara zinazolalamikiwa na baadhi ya watu… kwa sababu wageni wanaoruhusiwa ni watano pekee, naamini kila timu itahakikisha kuwa inawasajili wachezaji wakali na ambao hawataishia kuwa watazamaji majukwaani huku mwisho wa siku wakilipwa fedha nyingi.
"Kwa sababu hiyo, ushindani wa kuwania kupangwa katika kila timu na pia ule wa ndani ya uwanja wakati wa mechi utaongezeka. Mwishowe kiwango chetu kitapanda," anasema Nyoni, ambaye pia alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliokuwa wakiibeba timu ya taifa, Taifa Stars, wakati ilipokuwa chini ya kocha aliyemaliza mkataba wake mwezi uliopita, Mbrazili Marcio Maximo.
"Faida nyingine ni kwamba, wageni legelege hawatawazibia nafasi wachezaji chipukizi katika usajili. Hili litawasaidia wadogo wenye vipaji kupata nafasi ya kucheza na pengine kuitwa katika timu ya taifa ili baadaye wasaidie katika kuunda kikosi kikali cha nyota chipukizi kama ilivyokuwa kwa timu zilizojaza yosso wengi za Ghana na Ujerumani katika fainali za Kombe la Dunia.
"Enzi za kusajili wageni wenye majina maarufu, lakini wasiokuwa na kiwango kinachoendana na sifa na bei wanazonunuliwa sasa zitafikia mwisho. Azam husajili wageni wakali tupu na kuna programu nzuri za kukuza vijana ambao baadaye hupandishwa katika timu kubwa.
"Ni kwa sababu kama hizi, zinazosaidia kukua kwa kiwango cha soka nchini, ndipo binafsi ninapoona kwamba TFF iko sahihi kuishikia bango kanuni hiyo inayokataza timu za ligi kuu kusajili wageni zaidi ya watano," anasema Nyoni, mkali aliyevutiwa na kiungo ‘yosso’ Dede Ayew wa Ghana kutokana na kiwango cha juu alichoonyesha wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini; lakini aliyekerwa na utabiri wa pweza Paul katika mechi ya fainali ambao ulikuwa wa kweli na hatimaye kuipa ubingwa Hispania dhidi ya timu aliyotarajia itwae kombe hilo ya Uholanzi.
AGOSTI 21
Nyoni anasema katika msimu ujao wa ligi kuu ya Bara itakayoanza kutimua vumbi Agosti 21, kwa mara ya kwanza, klabu yake ya Azam iliyomaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita baada ya kuzidiwa na timu za Simba na Yanga, itamaliza tambo za klabu hizo kongwe kwa kutwaa ubingwa wa 2010/2011.
Akifafanua sababu za kuwa na matumaini hayo, Nyoni anasema kuwa timu yao (Azam) imesajili kikosi cha mwaka huu kwa umakini zaidi kulinganisha na wapinzani wao wote na kwamba kama ni ‘fitna’, haamini kuwa zitawakwaza uwanjani kutokana na maandalizi yao makali katika fukwe za peninsula ya Kigamboni na pia visiwani Zanzibar.
"Kama nilivyosema awali, timu yetu inaangalia zaidi uwezo wa wachezaji na si majina yao. Kila aliyejumuishwa kikosini, ameangaliwa kwa uwezo wake na maandalizi yetu ndiyo yanayonipa imani zaidi kwamba ubingwa wa msimu ujao utaangukia mikononi mwetu," anasema Nyoni, pengine akikunwa na yosso tele wenye vipaji kikosini mwao na pia usajili wao mpya uliowaleta klabuni kwao nyota kadhaa, wakiwemo Mrisho Ngassa kutoka Yanga, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Jabiri Aziz kutoka Simba na Patrick Mafisango kutoka kwa mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, klabu ya APR ya Rwanda.
chanzi ni mtandao wa Azam football club na Habari kwa hisani ya Gazeti la LeteRaha
Comments