Kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa nchini Tanzania, mjasiriamali na mbunifu wa mavazi na mwanaharakati kwenye sekta ya utamaduni, Bi. Sophia Urio, kwa kuzingatia ushauri wa wataalam ambao nao pia ni wajasiriamali, amefanya ubunifu wa kipekee na kuanzisha mtindo mpya wa mavazi, unaotambulika kwa jina la “Tinga Tinga Fashions”.
“Nilipewa ushauri wa kufanya kitu kipya, wazo jipya, kwa kuzingatia kwamba wabunifu wengi wa mavazi hapa nchini wanarudia mambo yale yale ya zamani, na wengi wanaiga mitindo ya nje ya nchi. Sanaa ya Tinga Tinga iliasiliwa hapa nchini, ni fahari yetu.
Tunapofanya ubunifu tuzingatie kwanza hazina iliyopo nchini, kabla ya kutoka nje ya nchi. Mbona wabunifu wa nje wanazingatia urithi wao, iweje sisi tuwe waigizaji kila siku?” alisema Bi. Sophia.
Bi. Sophia amesema, alichokifanya ni kuunganisha sanaa ya michoro ya Tinga Tinga, iliyoanzishwa na mchoraji mahiri, marehemu Mzee Saidi Tinga Tinga, na sanaa ya ubunifu wa mavazi, kwa kuzingatia mila na tamaduni za Kitanzania.
“Nimeunganisha sanaa ya uchoraji, kupitia mtindo wa Tinga Tinga, na sanaa ya ubunifu wa mavazi, kwa kuzingatia mitindo ya Kitanzania na Kiafrika, hivyo nikapata kitu kinachoitwa Tinga Tinga Fashions. Hii ndiyo asili ya mtindo huu mpya kabisa, ambao ni muunganisho wa aina mbili sanaa zenye historia moja,” aliongeza Bi. Sophia.
Akizingatia hazina kubwa ya utamaduni iliyoasisiwa na marehemu Mzee Saidi Tinga Tinga, pamoja na wanafunzi wake walioendeleza fani hiyo, Bi. Sophia amesema amewaalika warithi wa marehemu Saidi Tinga Tinga pamoja na wachoraji wanaoendeleza fani hiyo kushiriki kwenye uzinduzi huo, ambao utafanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Utamaduni cha Makumbusho (Makumbusho Culture Centre), kilichopo Makumbusho, Kijitonyama, Dar es Salaam, kuanzia saa 12 jioni, Jumamosi, Agosti 7, 2010.
Amesema ameamua kuwaalika wadau wa sanaa ya Tinga Tinga ili kuwaenzi kutokana na mchango wao mkubwa kwenye sanaa Tanzania, pia kuchangia uhamasishaji wa kazi yao ya kisanii yenye kiwango bora ili ithaminiwe na kufahamika zaidi miongoni mwa Watanzania. Wasanii wa Tinga Tinga wataonesha kazi zao kwenye ukumbi huo wakati wa uzinduzi ili kuitangaza zaidi sanaa hiyo kwa kuwapatia elimu watazamaji.
Uzinduzi utapambwa na onesho la mavazi, ambapo mavazi tano ambayo yatabuniwa kwa madhumuni ya uzinduzi huo. Mavazi yataoneshwa kwenye jukwaa la Makumbusho Culture Centre, yakinadiwa na warembo mahiri ambao wameteuliwa kuonesha mavazi hayo. Bi. Sophia Urio, mbunifu wa mavazi hayo, amesema kwamba yataonesha hali halisi ya utamaduni wa mavazi wa Mtanzania, hususan, vazi linalostahili kuvaliwa na mwanamke anayezingatia mila na tamaduni za nchi yake.
Kwa upande wa burudani, onesho hilo litapambwa na wanamuziki wa bendi ya FM Academia (Wazee wa Ngwasuma), ambao watawaburudisha watazamaji ipasavyo. Pia, Bi. Sophia atasindikizwa na mbunifu chipukizi, Kemmy, kutoka kampuni ya “Binti Afrika”, ambaye naye ataonesha baadhi ya mavazi aliyoyabuni, akiwa na warembo watakaopanda jukwaani kuonesha mavazi hayo. Kiingilio kwa ajili ya uzinduzi huo pamoja na burudani zote zitakazokuwapo ni Shilingi za Kitanzania
Comments