Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, David Mgwassa, alisema kiwango walichopendekeza na kujadiliwa katika Baraza la walaji la Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kisitafsiriwe kuwa ni nauli halali, badala yake inaweza kukubalia au kukataliwa na serikali.
Juzi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alikataa ongezeko la nauli mpya kwa mabasi yaendayo kasi, alisema nauli hiyo itasababisha mzigo kwa wanbanchi na watumishi wa umma.
Alizitaka mamlaka husika zikiwemo TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi, Sumatra na UDA-RT kukaa haraka kurekebisha viwango hivyo.
Kiwango kilichopendekezwa na UDA ni Sh. 1,200 kwa safari ya njia kuu na Sh. 1,400 kwa njia ya pembeni, wanafunzi watalipa nusu ya kiasi hicho kwa kila barabara.
Hata hivyo, Mgwassa alisema kisheria wao walitakiwa kuandaa mchanganuo wa nauli ya utoaji huduma hiyo na kufikisha kwenye baraza la walaji ili wadau watoe maoni.
Katika kikao cha kujadili mapendekezo hayo kilichofanyika hivi karibuni, Sumatra na wadau mbalimbali walipinga nauli hizo wakisema ni gharama kumbwa ambayo wananchi wa kawaida hawawezi kumudu.
Sumatra ilishauri nauli ya usafiri wa kutumia mabasi hayo iwe sh. 400 hadi 500 katika kutimiza malengo ya serikali kusaidi wananchi kuondokana na kero ya usafiri jijini Dar es Salaam.
Chanzo: NIPASHE
Comments