Utangulizi
Nchi yetu
ina kingo za mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi ambamo watu
wanaishi kinyume cha sheria, huku wakiharibu mazingira na kuhatarisha
maisha yao. Kutokana na uhaba wa makazi, hali ni mbaya zaidi katika
mabonde ya Jiji la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto Msimbazi.
Serikali
za awamu zote, zimekuwa zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi wa maeneo
ya mabondeni wanaoishi katika maeneo hayo kinyume cha sheria lakini
mafanikio yamekuwa si ya kuridhisha.
Serikali
ya Awamu ya Tano, ambayo moja ya misingi yake mikuu ni utii wa sheria za
nchi, imeanza jitihada za kuwaondoa wakazi hawa. Tuliamua kuanza na
Bonde la Mto Msimbazi kwasababu ndiko kwenye watu wengi na athari kubwa.
Sababu zetu kuu za kufanya zoezi hili ni kusafisha mabonde na mito katika jiji la Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka ni:-
Kunusuru
maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi. Eneo la Bonde
la Mto Msimbazi lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu
tangu mwaka 1949 na baadaye 1979.
Kupanua
uwezo wa mito ya Dar es Salaam ili kupitisha maji ya mvua kwa kasi
kubwa, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa wakati wa
mvua nyingi; Kuzuia milipuko ya magonjwa, hasa ya kipindupindu, hasa
wakati wa mvua;
Kuzuia eneo hilo kuendelea kutumika kama maficho ya wahalifu na uhalifu;
Kutoa nafasi kwa Serikali kuandaa na kuendeleza eneo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;
Utaratibu wa Zoezi
Kabla ya
nyumba kubomolewa, taasisi hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba
anayokaa mkazi ina nyaraka za umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo
nyaraka hizo zina uhalali wowote. Nyumba ambazo zimethibitika kuwepo
katika maeneo yasiyostahili ndio zinawekwa alama X kuashiria kwamba
wakazi wanapaswa kuhama au kubomoa. Baada ya hapo, mkazi hupewa muda wa
kubomoa na kuhama mwenyewe. Kutokana na utaratibu huu, sehemu kubwa ya
nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa
wenyewe. Baada ya hapo, alama huwekwa kuonyesha mpaka wa bonde. Katika
zoezi hili, imebainika kwamba sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo ya
mabondeni ni wapangaji huku wamiliki wakikaa sehemu nyingine salama.
Serikali pia imeweka Dawati la Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi.(P.T)
Tathmini ya Zoezi
Jana,
terehe 7 Januari 2016, Mawaziri watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais; pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii), walifanya mkutano wa kutathmini zoezi la kuhamisha wakazi wa
mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam.
Mkutano
huo ulipokea ripoti ya timu ya wataalam wa Wizara mbalimbali,
inayoongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira,
ambayo, pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba sehemu kubwa ya
kubaini makazi yaliyojengwa kinyume cha Sheria katika Bonde la Mto
Msimbazi imekamilika. Ripoti ilieleza kwamba, hadi sasa, wananchi katika
nyumba 774 wamehama na nyumba hizo kubomolewa. Ilielezwa pia kwamba
kabla ya mkazi kuombwa kuhama, uhakiki kuhusu uhalali wa makazi
anayoishi hufanywa. Kutokana na uhakiki huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa
na hati halali za makazi na wakazi 119 walikuwa na leseni za makazi za
muda mfupi. Hawa watu hawakuhamishwa. Mawaziri walipokea maelezo kuhusu
changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi hilo. Baada ya
tafakuri na mjadala, Mawaziri hao walitoka na msimamo ufuatao, kama
uamuzi wa Serikali: -
1. Zoezi
la kuwaondoa wananchi waishio katika bonde la Mto Msimbazi (eneo
hatarishi) litaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na usumbufu
kwa wananchi;
2. Katika awamu hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu.
3. Kwa
wakati huu, watakaohitajika kuhama ni wale tu ambao makazi yao yamo
NDANI kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na kwenye
KINGO za mto;
4. Wale
watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma,
zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo,
hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga. Na watumishi wa
umma waliowamilikisha maeneo hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu na
kisheria;
5. Serikali, ndani ya siku tatu zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji umefanyika.
6.
Serikali itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na
baadhi ya wakazi wa mabondeni lakini pia itafuatilia kesi hizi ziishe
haraka ili taratibu zinazofuatia zifanyike;
7.
Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaoendesha
zoezi hili kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na kinyume na
misingi ya haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka alama za X zaidi ya mita
zilizowekwa kisheria. Limeanzishwa dawati la malalamiko katika Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupokea malalamiko au
maswali kuhusu zoezi hili.
8. Nyumba
na majengo ya miaka mingi, yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa
kwa Sheria zinazotekelezwa kwa zoezi hili, hayatabomolewa isipokuwa tu
pale maisha ya wakazi yapo hatarini. Wanaoishi katika makazi hayo
watapewa miongozo ya hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa;
9.
Serikali haina dhamira ya kubomoa mahoteli makubwa ya siku nyingi yaliyo
karibu na fukwe katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa mahoteli haya
watapewa masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa
Sheria.
10.
Serikali inaweka uratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake ili
hatua za utekelezaji wa sheria za nchi zisiwe chanzo cha taharuki katika
jamii.
11.
Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha
kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali
haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha
mvua kubwa maisha yao yapo hatarini. Itakumbukwa kwamba katika mafuriko
ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio mabondeni walipoteza maisha. Kwa
mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu zinatarajiwa
kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea katika miaka ya hivi
karibuni.
12.
Serikali inafuatilia kwa karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya
taarifa za wananchi wanaohitaji msaada maalum wa kibinadamu.
Suala la Mchungaji Getrude Rwakatare
Mkutano
ulipokea taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba ya Mchungaji
Rwakatare. Ilielezwa kwamba Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake
pahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo
zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume kabisa na Sheria tatu
muhimu. Pia ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za
kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini
ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali. Pale Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa
nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani. Wakati kesi inataka kuanza
kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa
wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe 11 Mei 2015, aliingia
makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya Baraza ya
kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza,
kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare. Makubaliano hayo yalisajiliwa
na Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei 2015. Mwanasheria huyo alificha
makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba 2015, yalipogundulika na
mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano ulielezwa kwamba Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu zote, alishaagiza
kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mwanasheria huyo.
Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na
taarifa zake zimekwishafikishwa TAKUKURU. Vilevile, Ofisi ya Makamu wa
Rais, iliiagiza Baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba
“makubaliano” kati yake na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu
yalipatikana na njia ya udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa tarehe
29 Disemba 2015.
Kuhusu Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano
pia ulijulishwa kuhusu hoja inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa
katika maeneo ya kuishi mabondeni lakini mradi wa DART umeachwa. Mkutano
ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira (kifungu 57 (2)) inatoa nafasi ya
kutolewa ruhusa kwa miradi/shughuli zenye maslahi ya taifa kufanyika
katika maeneo ya mabondeni, na kwamba Waziri mwenye dhamana ya mazingira
anaruhusiwa kutoa miongozo ya namna ya shughuli hizo zinavyoweza
kufanyika bila kuathiri mazingira. Mradi wa DART ulipata kibali hicho na
una mkataba na Baraza la Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya mazingira
zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016
Comments