Baada ya dili la uhamisho wa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania
Mbwana Samatta kusuasua kutoka klabu yake ya TP Mazembe kwenda klabu ya
Genk ya Ubeligiji, star huyo ameamua kurejea kwenye klabu yake hiyo ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ajili ya mazungumzo na tajiri wa
Mazembe Moise Katumbi kuhakikisha dili hilo linakamilika.
Manager wa Samatta Jamal Kisongo amesema, mbali na mazungumzo,
Samatta amerejea kwenye klabu yake ili aendelee kujifua hata kama
ikitokea boss huyo akamfungulia mlango wa kutokea basi awe yuko fiti
kuingia moja kwa moja kwenye timu kuliko kuendelea kukaa nyumbani.
“Tumeona ni vyema Samatta akarejea Mazembe katika kumpa presha na
kumsukuma Katumbi, amerejea kwenye kituo chake cha kazi na kumpa taarifa
Katumbi kuwa kama hato muuza kwenye klabu ya Genk basi yeye atamalizia
mkataba wake TP Mazembe na ataondoka mwezi April. Jambo ambalo kwa
hakika Katumbi hawezi kukubaliana nalo kwakuwa anajua Samatta akiondoka
mwezi April ataondoka bure na yeye atakuwa ameingia hasara”, amesema
Kisongo leo asubuhi wakati akihojiwa kwenye kipindi cha michezo cha
E-FM Radio.
“Lakini tumeona pia ni muhimu akaenda Mazembe ili awe anafanya
mazoezi hata kama ikitokea ameuzwa basi anaweza kutumika moja kwa moja
kwasababu atakuwa yuko fiti”.
“Mkataba wake na Genk unampa nafasi ya kujiunga mwezi January kama
Katumbi atamuuza, kama Katumbi atagoma, mkataba wake huohuo unampa
nafasi ya kuweza kujiunga katika majira ya joto (mwezi wa 7)”.
“Mbwana Samatta jina lake halijaingizwa kwenye orodha ya majina ya
wachezaji watakaocheza michuano ya klabu bingwa Afrika mwaka kuu,
Katumbi alishamuacha kwasababu anajua anamaliza mkataba mwaka huu na
atamuuza January. Kwa maana hiyo Mbwana hana faida kwenye klabu ya TP
Mazembe kwasababu ligi ya ndani ndiyo ligi pekee anaweza kucheza ambayo
hata wachezaji wengine wanaweza wakacheza vizuri tu”.
Mara baada ya Samatta kupata timu ambayo imeonesha kumuhitaji, boss
wa Mazembe amekuwa akitia ngumu kumuachia Samatta kutimkia Ubeligiji
badala yake amekuwa akimtafutia timu yeye mwenyewe huku akiwa na sababu
zake binafsi za kufanya hivyo lakini hana sababu za kimantiki za kumzuia
mchezaji huyo kujiunga na Genk.
Comments