UTEKELEZAJI wa upelekaji wa umeme katika vijiji kadhaa wilayani Magu umekamilika kwa asilimia 53, Bunge lilielezwa jana.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Charles Mwijage alisema wateja wapatao 1,887 wanatarajiwa kuunganishwa
umeme katika mradi huo utakaogharimu Sh bilioni 3.35.
Mwijage alikuwa akijibu swali la
Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu (CCM), aliyetaka kufahamu mradi wa
kupeleka umeme kwenye vijiji vya Yichobela/ Kinango toka Irungu na
Kabila toka Magu Mjini umefikia hatua gani.
Naibu Waziri alisema mradi wa kupeleka
umeme katika vijiji vya Yichobela na Kinango kutokea Irungu unahusisha
ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 umbali wa kilometa
nane.
"Ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti
0.4 umbali wa kilometa saba na ufungaji wa transfoma tano. Mradi huu
unatekelezwa na Mkandarasi Chico-CCC (BJ) JV Limited kwa ufadhili wa
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili,"
alieleza Naibu Waziri.
Alisema mpaka sasa ujenzi wa njia ya
umeme ya msongo wa kilovoti 33 umekamilika kwa asilimia 100; kazi ya
upimaji na michoro ya njia ya msongo wa kilovoti 0.4 imekamilika kwa
asilimia 100 na mkandarasi ameshaleta nguzo zote na transfoma tano
kumalizia kazi zilizosalia.
"Mradi wa umeme kutokea Magu Mjini
kuelekea Kabila kupitia Itumbili, Kitongo, Sukuma Sekondari, Lumeji,
Busalanga, Nhaya Sekondari, Nhaya Senta na Mwashepi unahusisha ujenzi wa
njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 umbali wa kilometa 28; ujenzi wa
njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 umbali wa kilometa 10 na
ufungaji wa transfoma 18," alieleza Mwijage.(HABARI LEO)
Comments