WANASIASA wameambiwa kuwa ubunge hautatokana na kiungo cha albino na kuachana na fikra hizo potofu.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Perreira Ame Silima amekiri bungeni
kuwa ni kweli zipo taarifa kuwa baadhi ya wanasiasa wanahusishwa na
imani potofu za kutumia viungo vya binadamu ili kupata madaraka.
"Ni kweli
habari ziko zinazungumzwa kuwa wanasiasa fulani na zinaibuka wakati
kama huu ambako kuna joto kali la Uchaguzi Mkuu," alisema Silima na
kuongeza: "Ubunge hautatokana na kiungo cha albino."
Alikuwa
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CCM),
aliyesema vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vinaeleza kuwa wapo
wanasiasa wanaotumia viungo vya albino kusaka umaarufu.
"Vyombo
hivi vya habari vya ndani na nje ya nchi vinaeleza kuwa wapo wanasiasa
waokwenda kwa waganga na kutumia viungo vya albino kujitafutia umaarufu.
Kwa nini serikali isiwabane waandishi hawa ili iwataje wanasiasa hao
ili wasiohusika wasitiwe doa," alihoji mbunge huyo wa Rombo.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada
kubwa katika kukabiliana na tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu, na
kuwa lazima jamii kuanzia ngazi ya familia ibadili fikra zao.
Alisema
haiwezekani albino wauawe katika baadhi ya mikoa au eneo fulani tu la
nchi, hivyo elimu inahitajika kwa watu husika na kuwa serikali
itaendelea kuchukua hatua zikiwamo za kuielimisha jamii.
Aidha,
alisema kifaa maalumu kitakachofungwa kwa albino ili kufuatilia mienendo
yao, kinaendelea kufanyiwa kazi na serikali ili kufahamu kama
teknolojia kinafanya kazi na pia kufahamu kama ni salama.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), Jenista Mhagama, alisema serikali haijalidanganya Bunge kuhusu
kifaa hicho, na kuwataka wabunge kuungana pamoja na serikali katika
kukomesha mauaji hayo yanayolitia aibu Taifa.
Akijibu
swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Philipa Mturano (Chadema),
Silima alisema mpaka sasa watu 15 wa mauaji ya albino, wamekamatwa,
kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.(HABARI LEO)
(KILONGE)
Comments