WAZIRI Nyalandu akikagua gwaride la askari wa wanyamapori wakati akiwa kwenye moja ya ziara zake.
Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema kauli zilizotolewa Bungeni na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, ni za kutapatapa na zimejaa ukosefu wa busara na uzushi.
Amesema mbunge kusimama bungeni na kutoa kashfa badala ya kueleza masuala ya kisera au kiutendaji ni kupungukiwa busara na jamii haina budi kumpuuza.
Akichangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni juzi, Nassari alisema Nyalandu kazi yake kubwa ni kuzunguka katika mapori ya akiba na kupiga picha na askari pamoja na kushangaa mbwa wa kizungu na kupokea ndege, helkopta za msaada. Alisema utendaji huo na mawaziri wengine unaweza ukawa ni ishara ya serikali iliyochoka.
Hata
hivyo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Nyalandu alisema
Nassari anapaswa kuwakilisha na kutetea wapigakura wake kwa hoja badala
ya kuropoka masuala ambayo hayana tija.
Alisema
kauli zinazotolewa na wapinzani bungeni akiwemo Nassari kuishutumu
serikali kuwa imechoka na kujaribu kuichonganisha na wananchi, kamwe
hakuwezi kuikatisha tamaa kwa kuwa uzushi kwa upinzani ni jambo la
kawaida.
Alikumbusha
kuwa mapema mwaka huu alifanya ziara wilayani Arumeru ikiwemo jimbo la
Nassari kutatua mgogoro baina ya wananchi na hifadhi, ambapo mbunge huyo
alimtia moyo na kumtaka kupuuza kauli za kukatisha tamaa zinazotolewa
dhidi yake.
“Hizi
kauli za Nassari ni za kitoto na haziwezi kuleta tija kwa wapigakura
wake…asimame kuzungumzia utendaji na masuala ya kisera sio kashfa ambazo
hazipo…Namshauri awatumikie wapiga kura wake.
Nilifanya
ziara jimboni kwake kutatua mgogoro na alinitia moyo kutokata tamaa na
kauli za watu wanaonibeza na kunipongeza kwa utendaji kazi wangu,”
alisema Nyalandu katika taarifa yake.
Taarifa
hiyo pia ilikariri kauli ya Nassari aliyoitoa katika mkutano wa viongozi
wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, ambapo mbunge huyo na Aggrey Mwanry
(Siha) walihudhuria akisema: “Naomba kukutia moyo kwani anayefanya kazi
ya Mungu atapata nguvu, nikisikia mtu bungeni anasema wewe ni waziri
mzigo, mimi nitaruka juu na kumwangukia vibaya.”
Imeeleza
kuwa mafanikio makubwa ambayo wizara hiyo imepata kwa kumaliza migogoro
ya ardhi mingi kwa muda mfupi wakati alipotembelea mapori ya akiba na
hifadhi za taifa zenye migogoro ya ardhi na wananchi na kuipatia
ufumbuzi.
Akiwa huko amekuwa na utaratibu wa kuzungumza na askari wa wanyamapori pamoja na wananchi kusikiliza kero zinazowakabili.
Miongoni
mwa maeneo ambayo Nyalandu ametembelea ni wilaya ya Mbarali mkoani
Mbeya, ambako kulikuwa na mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa vijiji 21
na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, uliodumu kwa miaka zaidi ya mitano bila
kupatiwa ufumbuzi.
Nyalandu
alimaliza mgogoro huo kwa kuruhusu wananchi wa vijiji hivyo kuendelea na
maisha kama kawaida na kuagiza kufanyika kwa ukaguzi wa mipaka ya eneo
hilo upya.
Awali,
wananchi wa Mbarali waliishitaki serikali kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ambaye aliitaka serikali kumaliza
mgogoro huo kwa maslahi ya wananchi.
Maeneo
mengine yenye mgogoro ambayo Nyalandu alifanya ziara kwa lengo la kutoa
ufumbuzi ni Pori la Burigi wilayani Biharamulo, Iringa, Masasi, Lamadi
ambako alikutana na wafugaji kutoka mikoa yote nchini pamoja na Hifadhi
ya Taifa ya Saadani wilayani Bagamoyo ambako pia kulikuwa na mgogoro wa
ardhi.
“Ninapofanya
ziara natekeleza majukumu yangu kama waziri, siwezi kukaa ofisini
wakati kuna mgogoro baina ya wananchi na hifadhi za taifa na mapori ya
akiba…nina dhamana ya kushughulikia mambo haya hivyo, kauli za kitoto
kamwe haziwezi kunikatisha tamaa,” aliongeza Nyalandu.
Aidha,
aliongeza kuwa katika kuhakikisha serikali inashinda vita dhidi ya
ujangili, amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau wa uhifadhi na
kwa jitihada zake amefanikisha kupatikana kwa ndege, helkopta na vifaa
vingine ili kukabiliana na majangili.
Alisema
vifaa hivyo ikiwemo ndege, magari, helkopta, silaha na vitendea kazi
vingine hukabidhiwa kwake na baadaye huvikabidhi kwa watendaji wake kwa
ajili ya kukagiwiwa kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
“Tumeanzisha
vita dhidi ya majangili hivyo ni lazima tuwe na vitedea kazi vya
kutosha, nimefanya jitihada za kupata helkopta, ndege, silaha za kisasa,
magari na juzi Marekani imetupa mbwa maalumu ambao tutawatumia pia
kwenye viwanja vya ndege na bandarini kwa usalama zaidi.
“Sasa
Nassari anaumia kuona hizi jitihada zetu kama serikali katika kulinda
rasilimali zetu au alitaka akabidhiwe yeye,” alihoji Nyalandu.
Akizungumza
kupiga picha na askari wa wanyamapori, Nyalandu aliwapuuza watu wenye
mawazo tofauti akisema si jambo baya kufurahi na wapiganaji wake, ambao
wamekuwa wakitumia muda mwingi wa maisha yao msituni.
Alisema
amekuwa na utaratibu wa kufurahi pamoja, kula na kunywa na askari wa
wanyamapori pindi anapofanya ziara zake katika hifadhi na mapori ya
akiba.
“Watu
wenye nia mbaya siku zote ndio wamekuwa na imani potofu, ninapofanya
ziara kwanza nawafikiria wapiganaji wetu wanaoishi msituni kukabiliana
na majangili hatari…siwezi kwenda huko na kukunja sura kama tuna ugomvi
bali baada ya kupeana maagizo ya kazi tunakuwa kitu kimoja, tunafurahi
na kutiana moyo ili kuongeza ari ya kulinda rasilimali za taifa. Kauli
zingine zinasikitisha mno,” alisema.
HABRI KATIKA PICHA
HABRI KATIKA PICHA
Waziri
Nyalandu akikagua nyara a serikali zilizokamatwa kutoka kwa majangili
alipokagua moja ya mbuga za wanyama kwenye moja ya ziara zake hivu
karibuni
NYALANDU
akiwa kwenye picha ya pamoja na askari wa wanyamapori, maofisa na
wafanyakazi wa Pori la Selous, muda mfupi baada ya kuzungumza nao na
kupeana mikakati ya kiutendaji.
Waziri
Nyalandu akikagua meno ya tembo yaliyokamatwa kutoka kwa majangili
kufuatia operesheni zinazofanywa na askari wa wanyamapori.
WAZIRI
Nyalandu (katikati) akiwa amezungukwa na wananchi wilayani Chemba
alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa kijiji na
hifadhi ya misitu.
WAZIRI
Nyalandu akiwa na wanafunzi wa Sekondari ya Selous wakati alipokuwa
kwenye ziara ya kukagua shughuli za uhifadhi na vita dhidi ya ujangili,
ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi shuleni hapo.
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akila chakula cha mchana na
wanafunzi wa sekondari ya Selous, iliyopo Kijiji cha Lukuyu Sekamaganga
wilayani Namtumbo, Ruvuma.
WAZIRI
Nyalandu akiwa katika picha ya pamoja na vijana wanaounda vikundi vya
ulinzi kwa lengo la kukabiliana na ujangili kwenye maeneo ya Pori la
Akiba la Selous wilayani Namtumbo.
Comments