Tanzania Breweries Limited (TBL) imetangaza bei mpya ya vilaji vyake. Afisa Uhusiano wa TBL, Doris Malulu, amesema kwamba bei hiyo mpya itaanza kutumika kuanzia leo.
Malulu alisisitiza wauzaji wa rejareja wauze vilaji hivyo kwa bei iliyoidhinishwa na TBL ili kuepuka dhuluma na kuwaongezea mzigo wanywaji.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba kama bei hiyo mpya itazingatiwa hasa kwa jiji la Dar es Salaam, huenda isiwe ni jambo la ajabu kwa sababu baa nyingi tayari zilianza kutumia bei hiyo tangu Julai, mwaka jana.
TBL walijaribu kupambana na walanguzi hao tangu mwaka jana kwa kusambaza vibao ili vibandikwe kwenye mabaa na kuonyesha bei halisi, lakini baadhi ya mabaa walivitupilia mbali na kuuza kwa bei wanazotaka wao.
Kwa mujibu wa bei hiyo mpya iliyotangazwa na TBL jana, bia za Safari, Kilimanjaro, Tusker, Bingwa na Balimi ambazo zinauzwa kwa ujazo wa mililita 500, sasa bei yake halisi ni Sh1,400 badala ya bei ya zamani ya sh1,300.
Aina ya bia hizo, ambazo zinauzwa katika ujazo wa mililita 330, badala ya Sh1,100 sasa zitauzwa kwa Sh.1,200, isipokuwa Balimi ambayo itakuwa Sh1,000.
Akifafanua zaidi juu ya bei hiyo mpya, Malulu alisema kwa ujumla bei ya bia zote kwa rejareja zimeongezeka kwa Sh100.
Bei mpya ya aina nyingine za bia za TBL pamoja na kiwango cha ujazo wa mililita kwenye mabano ni Ndovu Special Malt (375) Sh1,400, Castle Lager (500) Sh1,500, (330) 1,300, Castle Milk Stout (500) Sh1,600 na (375) Sh1,300.
Guinness (500) Sh1,800, Redd's Premium Cold (330) na (375) Sh1,400 wakati bia zinazopatikana zaidi Kanda ya Kaskazini za Eagle (500) Sh1,100 na (300) Sh700.
Kwa mujibu wa bei hizo mpya, Kinyaji kisicho na pombe cha Guinness Malt (300) kitauzwa kwa Sh900 na (330) Sh1,100.
Malulu alizitaja sababu za kupanda kwa gharama za vinywaji wanavyozalisha kuwa ni kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji.
"Bei zimepanda kutokana na sababu mbalimbali miongoni ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za malighafi, usafirishaji, kupanda kwa bei ya mafuta na kushuka kwa thamani ya shilingi," alisema Malulu.
Alisisitiza kwamba matangazo ya viwango vipya vya bei za jumla na rejareja tayari wameyachapishwa na yanasambazwa kwenye baa na mawakala wao kote nchini
Comments