Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana aliugua ghafla akiwa katika maandamano ya kumsindikiza mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa baada ya kuchukua fomu za kugombea urais katika Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC).
Mbowe alishiriki katika maandamano yaliyoanzia Makao Makuu ya CUF yaliyopo Buguruni wilayani Ilala kuelekea NEC na baada ya Lowassa kuchukua fomu, mwenyekiti huyo aliendelea na msafara kwenda Kinondoni yalipo makao makuu ya Chadema.
Wakiwa njiani Mbowe na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu walikuwa wamechomoza kwenye gari wakiwapungia wananchi waliojitokeza kwenye maandamano hayo.
Hali ya
Mbowe ilibadilika ghafla na aliamua kushuka juu ya gari na kukaa katika
kiti, ndipo Lissu na watu waliokuwamo kwenye gari hilo wakaanza kumpatia
huduma ya kwanza kwa kumfungua vifungo vya shati lake katika eneo la
Kinondoni kwa Manyanya.
Wakati
hali ya Mbowe ilipoanza kubadilika msafara wa Lowassa ulikuwa ukielekea
katika Uwanja wa Biafra, Kinondoni na magari yalikuwa yakitembea mwendo
mdogo kutokana na maelfu ya watu waliokuwa wakiandamana.
Wakati
maandamano hayo yakiendelea, gari lililombeba Mbowe likiwa na walinzi wa
Chadema walioning’inia milangoni, lilichomoka katika msafara huo ambao
ulikuwa umeingia Barabara ya Kawawa na lilikunja kona katika barabara ya
kuelekea Mahakama ya Kinondoni kwa ajili ya kumwahisha hospitali na
taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa lilielekea katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Akizungumzia hali hiyo, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema kuwa Mbowe yuko salama na anaendelea vizuri.
“Ni uchovu, uchovu, uchovu tu but he is out of danger (hayuko katika hali ya hatari),” alisema Lissu.
Ofisa
Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema walimpokea Mbowe saa 11 jioni
na alikuwa anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo, hata hivyo
hakutaka kuweka wazi ugonjwa uliokuwa unamsumbua.
Chanzo:Mwananchi
Comments