Wakati wachezaji wa soka la kulipwa wakiwa kwenye mchakato wa
kusajiliwa kwenye timu mpya kuna vitu vingi sana hutokea ambavyo
kimsingi vinakamilisha mchakato wa usajili wa mchezaji husika toka timu
moja kwenda timu nyingine.
Moja kati ya vitu vya msingi ni vipimo vya afya ambavyo wakati
mwingine huweza kuzuia usajili kufanyika kwa sababu timu hutumia fedha
nyingi kumsajili mchezaji na hivyo lazima uhakika wa uwezo wa mchezaji
wa kuitumikia klabu ipasavyo .
Mara nyingi huwa inasikika kuwa mchezaji anafanyiwa vipimo vya afya
lakini si watu wengi wanafahamu vipimo vya afya kwenye usajili
vinahusisha nini.
Unaweza kujiuliza kwanini mchezaji anapimwa meno wakati anatumia
miguu kucheza mpira lakini ukweli ni kwamba vipimo vya meno hufanyika
ili kuhakikisha kuwa matatizo ya meno
hayatamsababishia mchezaji maumivu ambayo yanaweza kusababisha maambukizi mengine zaidi.
Vipimo vya macho.
Wachezaji hupimwa macho pia nah ii ni muhimu kwani kiungo hiki
kinatumika wakati mchezaji akiwa uwanjani na mtu ambaye ana matatizo ya
kuona mbali au karibu ni dhahiri kwamba uchezaji wake utaathiriwa kwa
njia moja au nyingine.
Mfano mzuri ni kipa David De Gea ambaye United ilimsajili ikiwa
inafahamu matatizo yake ya kutoona mbali na kwa sababu hiyo
wakamgharimia upasuaji wa kurekebisha macho yake.
Vipimo vya Presha na moyo.
Msukumo wa damu ni kitu muhimu sana kwa wachezaji hii ni kutokana na kazi wanayofanya na mazoezi kuhusisha matumizi ya
nishati na kutegemea msukumo wa damu kutoka maeneo mbalimbali ya mwili kuwa sawa na usio na matatizo yoyote .
Endapo ikigundulika kuwa mchezaji ana tatizo la presha ya kupanda au
ya kushuka hali inayosababisha msukumo wa damu ambao hauko vizuri basi
hawezi kusajiliwa kwa sababu anaweza kupata madhara makubwa zaidi.
Vipimo vya moyo pia ni muhimu kwani moyo ndio kiungo muhimu kwa
mchezaji kutokana na kutegemewa katika kusukuma damu na kuvumilia
mapambano ya uwanjani ,
mchezaji ambaye ana tatizo la moyo hawezi kuwa na uwezo wa kutumika uwanjani kwenye mechi au mazoezini kwa asilimia 100 .
Viungo.
Viungo vya mwili hususan miguu , mikono , na viungio vya maeneo hayo
ni muhimu pia hasa ukizingatia kuwa miguu kwa mfano ndio hasa jembe la
mchezaji .
Maeneo kama goti , kifundo cha mguu maarufu kama enka ,
kigimbi,kisigino , eneo la paja na misuli kwa jumla ni vitu ambavyo
vinatazamwa sana na kama haviko sawa basi mchezaji naye hawezi kuwa sawa
.
Afya ya mwili kwa Jumla.
Mchezaji pia hupimwa afya yake kwa jumla ambapo anatazamwa kama ana matatizo ya asili kama mpangilio usio wa kawaida wa homoni ,
kama ana tatizo la asili kama sickle
cell na magonjwa mengine ya kurithi ambayo yanaweza kumfanya asiwe
katika hali ya ushindani.
Kwa jumla timu huwa inahakikisha kuwa mchezaji yuko kwenye hali ya
afya ya asilimia mia moja ambayo itamfanya awe katika ubora wake wa juu
na hali ya kweza kumudu ushindani wa uwanjani
na kurejesha thamani ya fedha iliyotumika kumnunua kwani endapo mchezaji atanunuliwa huku akiwa na tatizo la afya halafu
akatumikia chini ya nusu ya muda wa mkataba wake itakuwa ni hasara
kubwa kwa klabu iliyomsajili na ndio maana mchezaji akifeli vipimo vya
afya hawezi kusajiliwa .
Comments