Skip to main content

Shy-Rose Bhanji Atangaza Nia Kuwania Ubunge Kinondoni


Shy-Rose Bhanji

• Asema mwaka 2010 ubunge unahitaji tafsiri mpya
• Aainisha maeneo nane atayoyafanyia kazi
• Kupiga vita utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana
• abainisha umuhimu wa ofisi kila kata ndani ya jimbo

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shy-Rose Sadruddin Bhanji ametangaza kujitosa

katika nafasi ya ubunge jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam kupitia CCM na

lengo lake kubwa ni kuwa kiungo muhimu katika jamii ya wanakinondoni.

Akitangaza azma yake ya kuomba ridhaa kwa wanachama wa CCM katika taarifa yake

kwa vyombo vya habari, Shy-Rose alisema kwa mtazamo wake neno ubunge kwa mwaka

2010 linahitaji tafsiri mpya kabisa. `…kwa sasa mbunge anatakiwa kuwa ni kiungo

cha jamii badala ya kuwa mwakilishi wa jimbo kama ilivyozoeleka` alifafanua

Shy-Rose.

`Mwaka 2010 ni mwaka wa mabadiliko na ndio maana nimeona kwamba ili kila

mwananchi kuweza kuwajibika, nafasi ya mbunge inahitaji kutafsiriwa upya ili

iendane na wakati na matatizo ambayo yanayotukakabili wananch` alisema.

Kwa maana hiyo amesema kwamba hata sifa za mbunge zinahitaji kutafsiriwa upya

kabisa, kwani majukumu yake yamebadilika kuendana na wakati. Ametaja baadhi ya

sifa hizo mpya ni kuwa mhamasishaji, kiungo muhimu, kufanya kazi usiku na mchana

na kuwa na ofisi katika kila kata ndani ya jimbo husika ili kuwafikia wananchi

kwa ukaribu zaidi.

`naomba nitoe tafsiri mpya ya neno ubunge..mbunge anatakiwa sasa awe ni kiungo

muhimu kati ya walio na kipato kikubwa, kipato cha kati na wasio na kipato kabisa

ili kwa pamoja jimbo liweze kupiga hatua za kimaendeleo. Mimi nitahakikisha

kwamba nina ofisi katika kila kata ili niweze kuwafikia wananchi wangu katika

kata zote kwani wakati napita kuomba kura ninawafuata na baada ya kufanikiwa

kutimiza azma yangu ni wakati wa kuendelea kuwafuata na si wao kunifuata`

alisema.

Kada huyo amesema sera yake kubwa itakuwa ni kumshirikisha kila mwananchi wa

Kinondoni katika shughuli za kuleta maendeleo ili kila mtu aweze kutoa maoni,

mawazo na mchango wa hali na mali katika kuleta maendeleo ya ukweli. Amesema hata

mwananchi ambaye atakuwa hana uwezo, atabeba tofali kutoka upande mmoja hadi

sehemu husika.

`nimeamua kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge kwa jimbo la hili ili niweze

kuleta mageuzi makubwa sana katika jimbo la Kinondoni…naomba mfahamu kwamba kila

mwananchi amebarikiwa akili, vipaji uwezo na Mwenyezi Mungu lakini

asiposhirikishwa hataweza kutoa mchango wake, hivyo mimi nitahakikisha kwamba

kila mmoja kwa uwezo wake na nafasi yake anachangia katika kuleta maendeleo`,

alifafanua.

Shy-Rose alibainisha mambo makubwa ambayo atayapigania kwa ari zaidi, nguvu zaidi

na kasi zaidi ni elimu, afya, ajira kwa vijana, kupiga vita utumiaji wa madawa ya

kuleta kwa vijana, kupigania haki za wasanii, kusaidia wajane katika kujikwamua

kiuchumi na kuleta msukumo mpya kabisa katika masuala ya mahusiano na jamii

ambayo kwa mtazamo wake eneo hili linahitaji msukumo mpya.

Shy-Rose amesema kwamba kutokana na uzoefu wa kazi zake tangu akiwa mwandishi wa

habari, mtangazaji na Meneja uhusiano katika sehemu alizofanyia kazi, anaamini

amekuwa mwanafunzi mzuri katika kutambua matatizo yanayoikabili nchi nzima na

hususan na jimbo la Kinondoni.

`kwa kuzingatia uzoefu wangu ndani ya jamii ya kitanzania na baada ya kufikiria

ni jinsi gani nitaweza kutumia akili, elimu yangu, uwezo, busara na vipaji vingi

nilivyojaliwa na Mwenyezi Mungu na nafasi yangu katika jamii, hatimaye nikafikia

uamuzi wa kujitosa kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hii.

`nimejifanyia tathmini ya kutosha, nimejiuliza maswali mengi na kutaka ushauri

kutoka kwa viongozi wa chama, familia yangu, marafiki, na wanachama wenzangu.

Nimefarijika kwa namna ya pekee walivyonihamasisha kutoka pande zote na ndiyo

sababu ya kupata ujasiri wa kujitokeza na kuomba kuteuliwa ili nitimize azma

yangu` alisema Shy-Rose.

Shy-Rose amesema ana kila sifa ya kujitosa na kuchaguliwa katika nafasi hiyo

kwani yeye amekulia kwenye chama tangu akiwa kwenye Umoja wa Vijana wa CCM sehemu

ambayo ni tanuri la kupika vijana kushika nafasi za uongozi na hatimaye kuiingia

kwenye chama na viungo vyake.

`Mkiangalia CV yangu mtaona kwamba nimekulia kwenye chama, sijapitia tu kwenye

chama, nimetokea ndani ya UVCCM, nimezunguka na viongozi mbalimbali wa chama na

serikali nchi nzima na nimejifunza masuala mengi sana ya kutumikia jamii, na

jinsi sera na ilani ya chama changu inavyofanya kazi zake za kila siku katika

kutumikia wananchi.`, aliongeza.

Shy-Rose amesema sababu ingine iliyompa ujasiri wa kujitokeza katika nafasi hiyo

ni kutokana na kauli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi akiwemo

Rais Jakaya Kikwete, za kuwataka wanawake kujitokeza katika kuwania nafasi za

uongozi ili Tanzania iweze kufikia hatua ya kuwa na wabunge asilimia 50 wakiwa ni

wanawake.

` kwa makusudi kabisa nimeamua kujitokeza kujitosa kwenye jimbo nikiamini kwamba

ninaweza…iwapo nitashinda nitakuwa ni mfano mzuri kwa vijana wenzangu ambao

wanapenda siasa lakini wametawaliwa na uoga wa kuingia hasa kwenye majimbo…kwangu

mimi nataka niwe mfano wa kuigwa na kuhamasisha wanawake hasa wanawake vijana

kuingia kwenye majimbo. Iwapo nitashinda basi mwaka 2015 vijana wengi zaidi

watajitokeza kuingia majimboni tofauti na hivi sasa mwamko wao ni mdogo`. Alisema

Shy-Rose ambaye kwa hivi sasa ni Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Benki ya NMB

Tanzania.

`kwa kuzingatia yote haya, nina kila sababu ya kuamini kwamba nina sifa za

kutosha za kuteuliwa katika nafasi ya ubunge kwa jimbo la Kinondoni hasa kwa sera

ya chama chetu ya kutaka kuwezesha wanawake kuingia katika nafasi za kutoa

maamuzi (decision making bodies). Naamini kwamba iwapo chama kitanipitisha na

hatimaye kushinda katika uchaguzi mkuu nitaweza pasipo shaka kushirikiana na

wananchi katika kuleta maendeleo makubwa ya kutatua kero za wananchi katika jimbo

hili.

Comments