Jana Juni 23, 2018 jioni Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amenusurika kifo baada ya mlipuko mkubwa kutokea kwenye jukwaa mjini Bulawayo alikokuwa akijinadi kwenye kampeni za uchaguzi mkuu nchini humo.
Mnangagwa ambaye aliongozana na mke wake pamoja na makamu wake wa Rais, Kembo Mohadi wote wameumia miguuni na tayari wamepelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa gazeti la serikali la The Herald limeeleza kuwa mlipuko huo ni jaribio la kutaka kumuua Rais Mnangagwa ambaye toka aingie madarakani mwaka jana baada ya kumpindua aliyekuwa Rais wa taifa hilo, Robert Mugabe amekuwa akipokea vitisho.
Shirika la Taifa la Utangazaji nchini Zimbabwe (ZBC) pia limeripoti kuwa mwenyekiti wa kitaifa wa Zanu PF Oppah Muchinguri-Kashiri, na Afisa mkuu wa kisiasa Engelbert Rugeje pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa ZBC walijeruhiwa
Kufuatia tukio hilo Mnangagwa amesema kuwa jaribio hilo lilipangwa na watu wenye nia mbaya juu yake ila siku zake hazikutimia.
“Nawapa pole watu wote waliojeruhiwa jioni ya leo (Jana jioni) hii ilikuwa ni mipango ya watu wenye lengo baya juu yangu na serikali mpya ya Zimbabwe, nadhani wakati wangu haujafika kwani mlipuko ulitokea karibu sana na mimi,“amesema Mnangagwa kupitia shirika la habari la Afrika Kusini (SABC).
Hata hivyo, tukio hilo pia limemgusa rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye amesema kuwa tofauti za kisiasa nchini humo zisilete uhasama bali ziimarishe demokrasia nchini humo.
Vyama vya upinzani na chama tawala cha Zanu-PF vipo kwenye kampeni ya uchaguzi mkuu wa urais na wabunge unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 mwezi Julai.
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps
Comments