BAADA ya mvutano na majadiliano ya hapa na pale, hatimaye kiungo wa Simba, Said Ndemla amekubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuwatumikia mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam.
Wiki iliyopita, Ndemla aliwagomea Simba kusaini mkataba baada ya kuwekewa mezani kiasi cha Sh. milioni 50.
Kiungo huyo ambaye alipandishwa kutoka timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20 (Simba B), alihusishwa na mipango ya kujiunga na Yanga na alikiri kufanya mazungumzo na mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara.
Taarifa kutoka ndani ya klabu zimesema kuwa Ndemla alikutana na mwekezaji na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji 'Mo' na kupewa kiasi ambacho alikihitaji na aliona ndio kinafanana na thamani yake.
"Tayari Ndemla ameshamalizana na Mo, sasa roho yangu imetulia, maana nilikuwa kila wakati namshauri awe na subira na asifanye uamuzi wa haraka, yeye ni mtoto wa Simba na anastahili kuendelea kubakia hapo," alisema mmoja wa viongozi wa Simba.
Comments