TIMU ya Singida United imeungana na Simba SC kwenda Nusu Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup baada ya ushindi wa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 na AFC Leopards jioni ya leo Uwanja wa Afraha, Nakuru nchini Kenya.
Shujaa wa Singida United leo alikuwa kipa wake, Manyika Peter Junior aliyeokoa penalti mbili, moja wakati wa dakika 90 za mchezo na nyingine kwenye mikwaju ya kuamua mshindi baada ya sare hiyo ya 0-0.
Na kwa ujumla, Manyika aliyerithi kipaji cha baba yake, Manyika Peter mkubwa aliyekuwa kipa wa Yanga na timu ya taifa miaka ya 1990 mwishoni hadi 2000 mwanzoni, alikuwa nyota wa mchezo wa leo baada ya kuokoa michomo mingi ya hatari kwenye mchezo huo.
Kwa ushindi huo, Singida United imelipa kisasi cha kutolewa na A.F.C. Leopards kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1 mwaka jana mjini Dar es Salaam katika hatua kama hii michuano hiyo ikifanyika kwa mara ya kwanza.
Tanzania Singida United 1 (4)Singida United ikicheza kwa mara ya kwanza chini ya kocha mpya, Hemed Morocco leo, sasa itakutana na Gor Mahia katika Nusu Fainali, wakati Simba SC iliyoitoa Kariobangi kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 0-0 itamenyana na Kakamega Homeboyz Juni 7.
Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup 2018 itafanyika Juni 10 na mshindi pamoja na kupata dola za Kimarekani 30,000 pia atapata nafasi ya kwenda kucheza na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England.
Mshindi wa pili atajipatia dola za Kimarekani 10,000, wa tatu dola 7, 500 na wa nne dola 5,000 wakati timu nyingine zitapewa kifuta jasho cha dola 2,500.
Comments