Tume ya Utumishi wa Mahakama imesema suala la majaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania wanaotuhumiwa kupokea zaidi ya Sh milioni 400 kutoka
katika Akaunti ya Tegeta Escrow, limefika kwenye tume hiyo na
linafanyiwa kazi.
Kwa utaratibu wa tume hiyo, baada ya uchunguzi taarifa hupelekwa kwa
rais ambaye baada ya kupitia mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti ya
uchunguzi, hutoa uamuzi.
Hayo yalielezwa jana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga,
katika banda la Tume ya Utumishi wa Mahakama katika maonyesho ya Wiki ya
Sheria yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
“Suala la majaji waliohusishwa katika Escrow limeshaletwa katika tume. Lipo na taratibu zinaendelea,” alisema Katanga.
Majaji wanaotuhumiwa kuingiziwa fedha hizo ni Profesa Eudes Ruhangisa (Sh milioni 404.25) na Aloysis Mujulizi (Sh milioni 40.4).
Katanga alisema dawa ya kumaliza mambo ni kuwa wazi kusema.
“Huo ni ukweli, inatakiwa uwepo uwazi zaidi…Tunatakiwa kuwa wazi,
hivi sasa tunataka kuweka mabango wananchi wajue jinsi ya kupata haki
kuepusha rushwa,” alisema.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Mahakama za Mwanzo, Warsha
Ng’humbu, aliyekuwapo katika banda la Kurugenzi ya Ukaguzi, Malalamiko
na Maadili, alisema kwa kuwa suala hilo limefika kwenye tume, maana yake
lilishapita katika Kamati ya Maadili ya Majaji.
Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Enzeel Mtei, alisema
tume hiyo inaundwa na wajumbe sita na ina jukumu la kumshauri rais juu
ya uteuzi wa Jaji Kiongozi au majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wengine ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu, Msajili wa
Mahakama ya Rufani na Msajili wa Mahakama Kuu au kutokuwa na uwezo kwa
watendaji hao.
Majukumu mengine ni kuchambua malalamiko dhidi ya majaji na kuchukua
hatua za utawala dhidi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi au
jaji na hatua zilizoainishwa katika Katiba.
Alisema kwa majaji wanaokwenda kinyume na maadili, tume hiyo
inachunguza madai hayo na kupeleka mapendekezo kwa rais kwa ajili ya
uamuzi.
Mtei alisema tuhuma zinazoelekezwa kwa mahakimu wa wilaya na mkoa
zinashughulikiwa na kamati ya mkoa na mahakimu wa mahakama za mwanzo
tuhuma zao zinashughulikiwa na kamati ya wilaya.
Chanzo: Mtanzania
Comments