Rais Jakaya Kikwete, amezindua sera mpya ya elimu ambayo pamoja na
mambo mengine, imehusisha hoja za Mbunge wa kuteuliwa (NCCR-Mageuzi),
James Mbatia, alizozitoa bungeni.
Mbatia aliibua katika mikutano tofauti ya Bunge mwaka juzi na jana,
akitaka serikali ipige marufuku matumizi ya vitabu tofauti vya mafunzo,
kwa vile vinachangia kufifisha kiwango cha elimu nchini.
Hoja za Mbatia aliyeingia bungeni na vitabu, akikosoa Sera ya Elimu
na kuibua mijadala ndani na nje ya Bunge na kumpatia umaarufu zaidi hasa
kisiasa.
Jana, Rais Kikwete alizindua sera hiyo na kusema inalenga kuchochea
uboreshaji wa elimu ikiwa ni pamoja kuruhusu matumizi ya kitabu cha aina
moja kwa shule zote.
“Sera hii inahimiza matumizi ya kitabu kimoja wakati wa kufundisha
ili kuzisaidia shule zote nchini badala ya kutumia vitabu vya aina
tofauti kama ilivyo sasa, hivyo kutakuwa na kitabu cha aina moja,”
alisema na kuongeza:
“Hatuwezi kuziendesha shule zetu kwa kutumia vitabu vya aina tofauti
ambapo kila shule inakuwa na vitabu vyake ambavyo wamevichagua, tumeamua
kuwa na kitabu kimoja kwa kila somo kitakachotumia na shule zote
nchini,” alisema.
Alisema sera hiyo itazishinikiza shule binafsi kuwa na ada nafuu
ambayo kila mzazi aweze kulipa na jamii inapaswa kutambua kuwa, elimu
ni huduma na siyo biashara.
Aliongeza kuwa huduma zote za binafsi zinapaswa kuwa na kiwango cha
ada kinachokubalika hivyo utafiti wa uendeshaji unapaswa kufanyika
kuelewa kiasi halisi kinachopaswa kulipa.
“Siyo wengine walipe shilingi milioni tano na wengine milioni sita,
tunataka tuwe na kiwango kinachoelewa, hatuwezi kuendelea kuongeza kiasi
cha ada bila ya kujua huduma zinazotolewa na shule kama inaendana na
ada inayolipishwa,” alisema.
Alisema serikali ilipanga kwa muda mrefu kubadili sera ya elimu kwa
sababu ni vigumu kuwa na maendeleo kama mfumo wa elimu sio mzuri.
Aliongeza kuwa, hakuna nchi duniani ambayo imeweza kutatua changamoto zote za elimu.
Alisema sera hiyo ya elimu imeandaliwa ili kutoa mwelekeo wa elimu na
mafunzo kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na
kiteknolojia.
Pia alisema changamoto za elimu na mafunzo kitaifa, kikanda na
kimataifa ili kuongeza fursa, ufanisi na ubora wa elimu na mafunzo na
kufikia viwango vya rasilimaliwatu kwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2025.
Alisema malengo ya sera ni kuwa na Watanzania walioelimika na wenye
maarifa na ujuzi kuweza kuchangia kwa haraka katika maendeleo ya Taifa
na kuhimili ushindani.
Alisema kupitia sera hiyo serikali itaweka utaratibu wa elimu ya
awali kuwa ya lazima na kutolewa kwa watoto wenye umri kati ya miaka
mitatu hadi mitano kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alisema mkoa
umejaribu kukamilisha maelekezo ya Rais ya kujenga maabara mpya ambapo
mpaka sasa zimejengwa 231.
Aidha, alisema mpaka sasa wanamaabara 412 katika shule za sekondari
na wanatarajia kupitia maabara hizo, wanafunzi watapata elimu ya
ushindani.
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa,
alisema kuwa, sera hiyo mpya ya elimu inalenga kuleta mabadiliko ya
kiuchumi na kijamii kwenye sekta hiyo.
Chanzo: NIPASHE
Comments