Serikali imeshusha bei ya umeme nchini kwa asilimia 2.21 kuanzia mwezi Machi mwaka huu.
Bei hiyo itatumika katika kipindi cha miezi mitatu wakati mapitio mapya yakiwa yanafanyika kulingana na mfumuko wa bei.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi, alisema
hatua hiyo imekuja baada ya kupitia gharama ya uzalishaji wa umeme kwa
kuzingatia mabadiliko ya bei ya mafuta, thamani ya shilingi ya Tanzania
na mfumuko wa bei.
Alisema kufuatia bei hiyo mpya watumiaji wa majumbani wamepunguziwa kwa shilingi nane kutoka Sh. 306 hadi Sh. 298.
Watumiaji wa kati wanaotumia umeme wa Volti 400, bei itashuka kutoka
Sh. 205 hadi Sh. 200 kwa uniti moja, sawa na punguzo la Shilingi tano
kwa uniti.
Wateja wakubwa walionganishwa katika msongo wa kati wa umeme,
watapunguziwa kwa Shilingi nne, ambapo watanunua Sh. 159 badala ya Sh.
163 ya awali.
Kwa wateja waliounganisha katika msongo mkubwa wa umeme kama migodi
na Shirika la Umeme Zanzibar, watapunguziwa Shilingi tatu, wamepunguziwa
gharama kutoka Sh. 159 hadi Sh. 156 kwa uniti moja.
“Kwa wateja wa majumbani wenye matumizi madogo ya wastani wa uniti 75
kwa mwezi, bei ya umeme haitabadilika kutokana na kundi hilo kuchangiwa
gharama na wateja wakubwa wa majumbani,” alisema.
Ngamlagosi alisema wateja hao wadogo wa majumbani wataendelea kulipia Sh. 100 kwa uniti moja.
Aidha akizungumzia namna walivyokokotoa gharama hizo, alisema katika
kupindi hicho Tanesco iliokoa Sh. Bilioni 57 baada ya uzalishaji kuwa wa
chini kwa mitambo ya uzalishaji inayotumia mafuta mazito na ya ndege..
Alisema katika kipindi hicho thamani ya shilingi ilishuka kwa wastani
wa asilimia 7.28, wakati mfumuko wa bei uliongeza mahitaji ya pato la
Tanesco kwa Sh. Bilioni 17.
Ngamlagosi gharama halisi ya pato la Tanesco kwa mwaka huo ulikuwa Sh. Bilioni 33.
Hata hivyo, alisema bei hiyo itadumu kwa muda wa miezi mitatu baada
ya kuwepo kwa kifungu cha kanuni kinachotaka bei elekezi katika huduma
hiyo kubadilika kila mara.
Alisisitiza yapo matumaini ya kushuka zaidi kwa bei ya umeme baada ya
kuanza kwa uzalishaji wa nishati hiyo kupitia mitambo ya Kinyerezi
pamoja na kufanya marekebisho kwa mitambo iliyopo kutoka kuendeshwa kwa
kutumia mafuta badala yake kutumia gesi.
Chanzo: NIPASHE
Comments