VIGOGO vya soka nchini, Simba na Yanga mwishoni mwa wiki hii vitakuwa na kazi nyingine pevu wakati vitakaposhuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu katika mechi za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Wakati Simba itashuka dimbani kesho kumenyana na Stand United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, watani wao Yanga watashuka dimbani kwenye uwanja huo Jumapili kumenyana na JKT Ruvu.
Mechi zote mbili zina umuhimu mkubwa kwa Simba na Yanga kutokana na matokeo mabaya ziliyoyapata katika mechi mbili za mwanzo.
Simba ilianza ligi hiyo kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Coastal Union kabla ya kulazimishwa sare nyingine dhidi ya Polisi Moro. Mechi zote mbili zilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Yanga ilianza ligi hiyo vibaya baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro kabla ya kuambulia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zitakazochezwa kesho, Polisi Moro itaikaribisha Kagera Sugar mjini Morogoro, Ndanda FC watakuwa wageni wa Coastal Union mjini Tanga, Prisons itaikaribisha Azam mjini Mbeya wakati Ruvu Shooting itacheza na Mbeya City mjini Ruvu mkoani Pwani.
Mechi nyingine itachezwa Jumapili kati ya Mtibwa Sugar na Mgambo JKT, zitakazomenyana mjini Turiani, Morogoro.
Comments