Kiungo mpya wa Azam FC,Frank Domayo ameanza kujifua na
mazoezi ya Gym,kwa ajili ya kujiandaa kuingia uwanjani Januari
mosi,baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuuguza
majeruhi ya nyama za paja.
Domayo amesajiliwa Azam msimu huu kama mchezaji huru baada ya
kumaliza mkataba wake na Yanga lakini alipojiunga na timu hiyo
alipelekwa nchini Afrika Kusini,kufanyiwa upasuaji wa mguu uliokuwa na
majeruhi aliyoyapata akiwa Yanga.
Mchezaji huyo alianza mazoezi ya Gym,Jumatano ya wiki hii na
Azam,ambapo alisema maendeleo ya mguu wake yapo vizuri tofauti na awali.
Wachezaji wa Azam huwa wanatumia Gym yao ya kisasa iliyopo kwenye
uwanja wao wa Azam Complex,Chamanzi nje kidogo ya Dar es Salaam.
“Nikijaliwa uzima nitahakikisha nafanya kile kilichowavutia viongozi
kunisajili,hivyo najituma kwa bidii ili niweze kuwa fiti,lakini naamini
nitafanya mambo makubwa nikishirikiana na wenzangu.”
Domayo ni kati ya wachezaji ambao usajili wao ulitikisa na kugusa
hisia za wadau wa soka nchini,jambo alilosema hatakubali heshima yake
ishuke kipindi atakaporudi uwanjani kucheza soka.
Comments