Serikali imefuta mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti kuanzia mwaka huu ili kuboresha kiwango cha elimu nchini.
Tamko hilo limetolewa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dkt.Shukuru Kawambwa wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ualimu
Tabora, kilichoko Manispaa ya Tabora.
Alisema kuanzia mwaka huu, Serikali imeyafuta mafunzo hayo ikiwa ni
mkakati maalumu wa kuboresha kiwango cha elimu ambapo walimu ambao
wataajiri wakufundisha shule za msingi na sekondari, watatakiwa kuwa na
elimu ya kiwango cha diploma na kuendelea.
Aliongeza kuwa, kuanzia sasa Wizara yake inataka kusimamia ubora wa
elimu na walimu ambao kuanzia mwaka huu, wale ambao wataajiriwa
kufundisha katika shule za msingi na sekondari, lazima wawe na elimu ya
kiwango cha diploma na wasiofikia kiwango hicho, watapewa fursa ya
kujiendeleza bila tatizo.
“Walimu wa shule za msingi na sekondari na wahitimu wa kidato cha
sita waliopata daraja la 1-3 na kuchaguliwa kujiunga na kozi maalumu ya
ualimu ngazi ya cheti, watapelekwa vyuoni kupata masomo ya diploma
katika vyuo maalumu vilivyoandaliwa.
“Ili kuhakikisha mpango huu unatekelezwa, Wizara inaandaa waraka
maalumu wamaelekezo ambao utatumwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote
nchini,” alisema Dkt. Kawambwa.
Awali, akijibu swali la mwanafunzi wa chuo hicho aliyetaka kujua
kwanini muda wakufanya mazoezi kwa vitendo (BTP) umepunguzwa na kuwa
wiki tatu badala ya siku 60, Dkt. Kawambwa alisema utaratibu huo ni wa
dharura kutokana na uhaba wa fedha.
Alisema Serikali itajitahidi kurekebisha hali hiyo kadri hali ya
kifedha itakavyoruhusu ambapo akizungumzia ombi la kuongezwa posho
kutoka sh. 4,500 wanazolipwa sasa hadi sh.7,500 ambazo wanalipwa
wanafunzi wa ngazi ya Shahada, aliahidi kulifanyia kazi suala hilo
katika Bajeti ya Wizara.
“Nawaomba wanafunzi wote wa vyuo vya ualimu, kuhakikisha mnafaulu
masomo yote mnayofundishwa chuoni ili muweze kuajiriwa serikalini
vinginevyo mtakaa benchi,” alisema.
Dkt.Kawambwa alisema wakati anaingia katika Wizara hiyo, alisema
hataajiri walimu waliofeli, hivyo ataendelea na msimamo huo kwa nia
njema, hivyo wanafunzi waliopo shuleni wanapaswa kufaulu masomo yao na
ya ziada ili waweze kuajiriwa.
Chanzo: Majira.
Comments