Meya wa Manispaa ya Tabora, Gulam Hussein Dewji ameshushiwa tuhuma
nzito za kuidanganya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa
kushindwa kutangaza mali anazozimikiki zikiwamo pikipiki 422, licha ya
kutakiwa kufanya hivyo kisheria.
Sheria Namba 5 ya mwaka 2001 ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inamtaka
kila kiongozi kujaza fomu za kutangaza mali zake na madeni na
kuziwasilisha kwenye Sekretarieti hiyo kila mwisho wa mwaka.
Meya huyo alisomewa mashtaka yake jana na Mwanasheria wa Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus mbele ya Mwenyekiti wa
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisi Msumi.
Mwanasheria huyo alisema kuwa meya huyo anatuhumiwa kutotamka baadhi
ya mali anazozimiliki na kuzitaja mali hizo kuwa ni pikipiki 422, magari
matatu, viwanja vitano na nyumba moja.
Cyriacus alisema kwamba meya huyo alishindwa kutangaza mali zake katika kipidi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2010 hadi 2013.
Tuhuma nyingine zinazomkabili meya huyo ni kuchukua Sh2.6 milioni
mali ya Manispaa ya Tabora kwa ajili ya safari yake kwenda nchini
Marekani.
“Mwaka 2012 meya huyo alipata mwaliko wa kwenda Marekani ambako
waliomwalika walimlipa gharama zote alipofika nchini humo lakini yeye
aliomba fedha katika manispaa hiyo kwa maelezo kwamba angezirejesha
baada ya kulipwa, lakini hadi sasa hajafanya hivyo,” alisema.
Akitoa ushahidi wa tuhuma hizo, Ofisa Maadili wa Sektetarieti hiyo,
Gerald Mwaitebele huku akiwasilisha vyaraka kwa Jaji Msumi, alisema kuwa
nyaraka kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zinaonyesha kuwa
mmiliki wa pikipiki na magari hayo ni Gulam Dewji.
“Nawasilisha matamko ya mali ambayo hayaonyeshi pikipiki 422, magari
matatu, viwanja vitano na nyumba moja inayomilikiwa na Gulam Hussein
Dewji,” alisema.
Alisema: “Licha ya mali hizi kumilikiwa na meya, lakini hazionekani
kwenye fomu za matangazo ya mali, huu ni udanganyifa mwenyekiti.”
Meya Dewji atapata muda wa kutoa utetezi wake katika kikao kijacho
cha baraza hilo, baada ya mashahidi watatu kutoa ushahidi wao mbele ya
tume hiyo
Jaji Msumi aliahirisha shauri hilo hadi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itakapopanga tarehe nyingine.
Huku serikali ikipambana kuzuia usafiri huo katika miji mikubwa, kumbe kuna watu ndani ya uongozi huo wakifanya shughuli hiyo…
Unafiki mkubwa huu…
Chanzo: Mwananchi.
Comments