Shirikisho
La kandanda la Nigeria NFF limefichua kwamba Shaibu Amodu ndiye
atakayechukua nafasi ya Stephen Keshi kama mkufunzi wa timu ya taifa ya
Nigeria.
Hatua hii imechukuliwa muda mfupi tu baada ya bw. Keshi
kuiongoza Nigeria katika mechi waliyoshinda kwa mabao 3-0 ingawa hakuwa
amepatiwa mkataba na kufufua matumaini ya Nigeria ya kufuzu kwa dimba la
kombe la Afrika litakaloandaliwa huko Morocco mwaka ujao.
Baada
ya kufanya mkutano wa dharura, shirikisho la kandanda nchini Nigeria
limeamua kumteua Amodu kuingoza timu ya taifa ya Nigeria katika mechi
zake mbili zitakazochezwa hapo Novemba katika juhudi zao za kujikatia
tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la Afrika.
Hata hivyo wamesema mkufunzi wa kudumu kutoka nchi za kigeni ataajiriwa baadaye.
Amodu anakabiliwa na wakati
mgumu kwani lazima ashinde mechi zote mbili watakazocheza ambapo mechi
moja watakuwa wageni wa timu ya taifa ya Jamhuri ya kidemokrasia ya
congo huku ya pili wakiwa wenyeji wa timu ya taifa ya Afrika kusini
endapo watafuzu.
Aidha mabingwa hao wa bara la Afrika wapo katika hatari kubwa ya kutofuzu na kushindwa kutetea taji lao.
Ushindi
walioupata dhidi ya Sudan ndio uliokuwa wao wa kwanza katika kundi A na
kuisaidia kupanda ngazi kutoka mwisho. Kwa sasa wako pointi tatu nyuma
ya Congo ambao wanashikilia nafasi ya pili.
"Kamati tendaji
imefanya uamuzi wa kumuachilia Keshi aondoke na kumpa Shaibu Amodu
mamlaka ya kuiongoza Nigeria katika mechi zake mbili zijazo," msemaji wa
NFF Ademola Olajire ameiambia BBC.
.
Comments