Jana (September 21) ni siku ambayo wenzetu nchini Kenya hawataisahau kabisa baada ya shambulio la kigaidi kuwakumba. Shambulio hilo lilitokea kwenye Mall ya Westgate jijini Nairobi ambapo watu weengi wameuawa na kujeruhiwa.
Watu waliokuwa kwenye Mall hiyo wakisaidiwa kutoka nje na Askari
Baada ya shambulio hilo, kundi la kigaidi la Al-shabaab lilitoa taarifa kwamba wao ndio wanahusika na shambulio hilo kupitia kituo cha habari cha BBC, na kwamba shambulio hilo limetokana na walichokifanya wanajeshi wa Kenya kwa Waislam wa Somalia. Westgate Mall (ni kama Mlimani City hapa Dar es Salaam) huwa inajaza wateja kutoka nchi mbalimbali Duniani.
Ni dhahiri kwamba ndugu zetu wamepata tabu sana kwa tukio hili, ni shambulio ambalo limefanya idadi ya waliofariki kufikia 39, zaidi ya watu 600 wameokolewa kutoka ndani. Inasemekana watu watano wamekamatwa kufatia tukio hilo na mmoja amefariki.
BBC Swahili pia imeandika:
Afisa mmoja mkuu wa kundi la kigaidi la Alshabaab, amefahamisha BBC kuwa kundi hilo ndilo limehusika na shambulizi dhidi ya duka la kifahari la Westage mjini Nairobi Kenya.
Kwa mujibu wa Afisa huyo mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa Kenya kwa kujihusisha na vita vya Somalia ambako wanajeshi wake wanakabiliana na kundi hilo.
Wanajeshi wa Kenya wamekuwa nchini humo tangu mwaka 2011 kama sehemu ya juhudi za muungano wa Afrika kutaka kurejesha uthabiti nchini Somalia.
Afisaa mkuu wa mambo ya ndani Kenya amesema idadi ya waliofariki ni kumi na moja lakini shirika la msalaba mwekundu linasema idadi hiyo imefika watu 30 huku zaidi ya hamsini wakijeruhiwa.
Taarifa kutoka Ikulu ya Rais Kenya zinasema kuwa mshukiwa mmoja aliyekamatwa alifariki kutokana na majeraha yake.
Wanamgambo wa Al Shabaab kupitia kwa mtandao wao wa Twitter , wanasema kuwa Kenya haikuchukulia kwa uzito onyo walilotoa kwa taifa hilo kwa hatua ya kuwapeleka wanajeshi wake nchini humo kupambana dhidi yao.
Kundi hilo limesema limekuwa likitoa onyo mara kwa mara kwa Kenya kuwa ikiwa haitaondoa vikosi vyake nchini Somalia, athari zitakuwa mbaya mno.
Kupitia mtandao wao wa Twitter, Al Shabaab limesema kuwa Kenya ilijidai kutosikia onyo hizo, na kuendelea kuwaua waisilamu wasio na hatia nchini Somalia.
Taarifa hiyo ya Twitter ilisema kuwa Shambulio la Westgate ni tone tu katika bahari ya mfano wa yanayowakumba wasomali nchini Somalia.
Taharuki ilianza hii leo saa saba mchana wakati watu wanaokisiwa kuwa kumi walipovamia jengo la kifahari la Westgate la kuwapiga risasi kiholela wakenya waliokuwa wanaendelea na shughuli zao za kawaida.
Kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu, takriban watu 30 walifariki kwa kupigwa risasi au kutokana na majeraha yao na wengine wengi wenye majeraha ya risasi kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Baadhi ya picha za watu waliojeruhiwa, waliofariki na za uokoaji uliokuwa unafanyika wakati wa tukio hilo:
Comments