Na Flora Martin Mwano
Rais wa Marekani Barack Obama anatarajia kuomba idhini ya bunge la nchi
hiyo ili aweze kufanikisha mkakati wa kuivamia kijeshi nchi ya Syria
inayotuhumiwa kwa matumizi ya silaha za kemikali dhidi ya raia wake.
Kwa mujibu wa katiba ya nchi yake, Rais Obama anayo haki ya kuliagiza
jeshi lake kuvamia Syria bila kuomba idhini ya bunge lakini jeshi hilo
halitatakiwa kukaa vitani kwa zaidi ya siku 60 ikiwa bunge
halikuidhinisha uvamizi.
Bunge la Congress linatarajiwa kupigia kura pendekezo hilo kabla ya
tarehe 9 mwezi huu na Rais Obama sasa anasema kuna umuhimu wa kuwa na
majadiliano kabla ya hatua za kijeshi kuchukuliwa.
Katika taarifa fupi iliyotolewa kwa waandishi wa habari mwishoni mwa
juma hili kwenye ikulu ya White House, Obama amesema jeshi la Marekani
lipo tayari kwa uvamizi ili kumuadabisha Bashar al-Assad kutokana na
majeshi yake kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Syria.
Marekani inasema ina uthibitisho kuwa majeshi ya serikali ya Damascus
yalitumia silaha hizo katika shambulizi la Agosti 21 pembezoni mwa mji
wa Damascus ambapo watu zaidi ya 1,000 walidaiwa kufa.
Serikali ya Syria imekuwa ikikanusha tuhuma zinazoelekezwa kwake na kuwataja waasi kuwa ndio waliotumia silaha za kemikali.
Comments