Siyo
kundi la Sungusungu, Polisi Jamii au askari wa makundi ya kiharakati au
kisiasa unaoweza kufahamu. Hakuna ofisi wala vikao wanavyokaa kusikiliza
mashtaka kabla ya uamuzi, mbaya zaidi hakuna anayejitambulisha kama
mfuasi wa baraza hilo, lakini linatoa hukumu na kutekeleza mauaji ya
kutisha.
Taarifa
zinaonyesha kuwa kwa mwaka jana pekee, wastani wa watu watatu walikuwa
wakiuawa kila wiki na kikundi hicho cha watu kinachofahamika kama Baraza
la Kimila katika Mkoa wa Simiyu, wakiwamo wanawake na watoto.
Wanachama
wa kikundi hicho maarufu Dagashida, hufahamiana muda wa kupokezana
'Mbiu'inaposikika kama ishara ya kuhudhuria tukio la utoaji wa hukumu.
Unaweza
kulinganisha na Kundi la Al-Shabaab, kwani baraza hilo hufanya maasi na
kusambaa msituni kwa muda wa siku zisizopungua tano wakihofia kutiwa
mbaroni na Jeshi la Polisi.
Baraza
hilo ni mfano wa kamati ya ulinzi au mahakama inayojiendesha kwa kufuata
miiko na kanuni zake katikati ya Serikali inayoendeshwa kwa utawala wa
sharia, likidaiwa kutoka Kabila la Wasukuma na jamii ya Kinyantuzu
waliopo Mkoa wa Simiyu.
Mmoja wa
maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu aliyeomba
kutotaja jina lake gazetini kwa sababu za siyo msemaji wa polisi
alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo ya kikatili akishauri atafutwe
mhusika ili atoe ufafanuzi kuhusu matukio hayo.
Hali ilivyo kwa sasa
Mwandishi
wa gazeti hili alifanikiwa kufika Vijiji vya Igangabilili, Nyamiswi,
Badugu, Shigala, Budalabujiga na Mikoma vilivyopo Wilaya za Itilima,
Bariadi, Busega na maeneo mengine mkoani humo.
Hofu
iliyopo siyo kwa wanakijiji tu, bali hata mgeni yeyote, wakiwamo
watumishi wa Serikali kama walimu, watakaoonekana kuwa tofauti na jamii
hiyo.
Taarifa zinaonyesha kuwa hata kwa mwandishi wa habari atakayebainika kuingilia utaratibu wao, atakutana na adhabu kali.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Kijiji cha Nyamiswi Kata ya Gambushi, Leah Muhami
anasema kuwa hali ni mbaya na kwamba mbali ya kuchoshwa na ukatili huo,
wanakijiji wamekuwa wakihofia kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa
kuogopa kuonekana wasaliti kwa baraza hilo wakihofu kugharimu maisha
yao.
"Yaani
wakikusikia unatoa taarifa zao polisi, lazima maisha yako yatakuwa
hatarini. Watakushughulikia na wanapofanya mauaji hutakiwi kuonekana
ukiwa na simu ya mkononi, "anasema Leah.Ukatili unavyofanyika
Katibu wa
CCM kutoka Wilaya ya Itilima, Jumaa Iadhi anasema ukatili huo, umekuwa
ukifanyika kwa kulipiza kisasi, ugomvi wa mirathi, mipaka ya ardhi na
njama zozote za kupangwa kwa namna yoyote, hata na watu wenye fedha.
"Kwa mtu
ambaye watamhisi au kupelekewa tuhuma za aina yoyote dhidi yake,
watapiga mbiu na kumweka katikati, kisha watampiga faini ya pesa ambazo
anatakiwa kuzitoa papo kwa papo,"anasema Iadhi.
Anasema
kuwa awali, baraza hilo walikuwa wakikusanya fedha na kuzipeleka kwenye
ujenzi wa visima, madarasa au madawati. "Wakati mwingine imeshakuwa ni
kama mradi wao wa kujipatia pesa za pombe, yaani ni ukatili
usiovumilika,"anasema Iadhi.
Mwingine
ni Michael Miraji, ambaye ni mkazi wa wilayani Bariadi anasema kuwa
sababu za kukithiri kwa matukio hayo ni jamii hizo kukosa huduma ya
Jeshi la Polisi, kukosekana kwa imani za kidini na elimu.
"Makanisa
na misikiti ni muhimu sana, mbali na mambo mengine kisaikolojia watu
wanajengewa tabia ya ustaarabu, lakini huku hadi mwenyekiti wa kijiji,
unakuta naye hana dini yoyote," anasema Miraji.
Anaongeza
kuwa umbali uliopo kati ya Kituo cha Polisi na kijiji ni takriban
kilometa 60. "Kwa umbali huo, askari wamekuwa wakikuta tukio tayari
limeshatokea, hivyo ni vigumu sana kudhibiti, labda Serikali iongeze
nguvu kwa mkoa huu wa Simiyu kama sehemu ya Operesheni Maalumu.
Matukio ya karibuni
Baadhi ya
matukio ya hivi karibuni ni pamoja lililotokea Kata ya Zagayu ambapo
wanawake wawili waliteketezwa kwa moto na baraza hilo kwa tuhuma za
ushirikina.
Mbali na
tukio hilo, tukio jingine ni la mauaji ya kuchomwa moto nyumba na
familia ya watu watatu katika Kijiji cha Budalabujiga.
Mmoja
kati ya maofisa usalama mkoani humo, ambaye hakuwa tayari kutajwa jina
lake anasema kuwa ingawa ukatili huo umepungua, lakini bado kuna
changamoto kubwa katika vijiji vya Kata ya N'hobora.
"Juzi
kuna wanakijiji watatu waliuawa kwa mapanga wakihusishwa na ushirikina,
pia kuna Kata ya Mkoma imekuwa na mauaji sana," anasema na
kuongeza:"Takwimu za matukio hayo zimeanza kupungua kutokana na juhudi
za utawala mpya wa Mkoa wa Simiyu ulioanzishwa hivi karibuni."
Anaongeza:
"Mwaka mmoja uliopita tulikuwa tunapokea taarifa za matukio ya vifo
viwili mpaka vitatu vya wanakijiji kuuawa kikatili kutoka ndani ya kila
kijiji, lakini kwa sasa zinaweza kumalizika siku tatu mpaka wiki
hatujasikia."
Mwalimu
wa Sekondari ya Biashara wilayani Bariadi, Mwangwa Bujiku anasema kuwa
ukatili huo umejenga hofu hata kwa walimu wanaopangiwa kwenda kufundisha
maeneo ya vijiji vya mkoa huo.
"Wenyeji
wa eneo hili hawapendi mtu anayekuwa tofauti na wao kiuchumi, hata
ukiongea Kiswahili wanaona unajidai. Kuna mwalimu alipangiwa Kata ya
Dutwa, alionekana kuishi tofauti wakamtengenezea kesi ya kutembea na
mwanafunzi," anasema Bujiku.
Anafafanua kuwa vijana wa baraza hilo waliamua kumpigia mbiu mwalimu huyo na kumpiga faini na kumfilisi kila kitu.
"Yule mwalimu akachukuliwa uhamisho na walikuwa wamepanga kumuua kabisa,"anasema.
Linatumika kwa visasi
Katibu wa
Umoja wa Wazazi mkoani humo, Fadhil Murani anasimulia akisema kuwa
mbaya zaidi baraza hilo limekuwa likitoa hukumu kwa kutumia hisia na
tuhuma zisizokuwa na uhakika.
"Halafu
mtuhumiwa wakishamweka katikati, haruhusiwi kujitetea wala kuzungumza
chochote, matokeo yake wanamchoma moto au wanamuua kwa mapanga,"anasema
Murani.
Anasimulia
kuwa asilimia kubwa ya vijana wa baraza hilo kwa sasa wanatumiwa na
watu wenye fedha katika ugomvi wa mipaka ya ardhi na mashamba.
"Mfano;
kama una adui yako ukapeleka pesa kidogo kwa wazee wa baraza hilo au
ukawanunulia pombe, halafu ukamshtaki mtu, lazima utasikia yule mtu
kavamiwa usiku na kuuawa kwa mapanga au watampigia Mbiu na kamchoma
moto,"anasema Murani.
Mmoja wa
wanavijiji kutoka Kata ya Mahuni, Deo Ngulyati anasema kuwa malengo
halisi ya kuwepo kwa baraza hilo yamepotea kwani limegeuka kuwa adui na
hasara katika ustawi wa jamii."Zamani lilikuwa ni baraza linalosaidia
ukuaji wa ustawi wa jamii na kuchochea maendeleo, walidhibiti migogoro,
walihamasishana kwenye misiba na majanga, kujenga huduma za kijamii na
walizuia uhalifu," alisema Ngulyati.
Changamoto kwa Jeshi la Polisi
Moja kati
ya changamoto kubwa na ya muda mrefu kwa Jeshi la Polisi mkoani Simiyu
ni hofu ya kuendelea kusambaa kwa mauaji na hukumu hizo.
Baadhi ya
Askari Polisi mkoani humo wamezungumza kwa nyakati tofauti juu ya
changamoto inayoendelea kujitokeza kupitia baraza hilo.
Mmoja
kati ya askari hao aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, anasema kuwa vijana
wa baraza hilo wakishatekeleza hukumu yao kwa raia hukimbilia msituni na
kujificha mfano wa Kundi la Al- Shabaab wakiwindana na polisi.
Anaongeza kuwa changamoto nyingine iliyopo ni viongozi wa Serikali za Mitaa na viongozi wa kisiasa kutotoa ushirikiano.
"Hakuna
mwanasiasa, awe diwani au mwenyekiti wa kijiji anayeingia bila
kushirikisha baraza hilo, kwa hivyo wanapokuwa madarakani wanakosa
ujasiri wa kuwakemea kwa maovu wanayoyafanya," anasema askari huyo.
Akichangia
hoja hiyo, askari mwingine katika kundi hilo anasema kuwa kwa sasa kuna
baadhi ya wanakijiji wameshaanza kutoa taarifa za matukio ya mauaji
yanapofanyika.
"Tukimkamta
mmoja wa vijana wa baraza hilo changamoto nyingine inajitokeza kwenye
ushahidi mahakamani. Hakuna mwanakijiji atakayekubali kusimama
mahakamani kutoa ushahidi, kwa hofu ya kuuawa. Inabidi mtuhumiwa aachiwe
huru kwa kukosa ushahidi," anasema askari huyo.
Itaendelea........................CHANZO MWANANCHI.
Comments