Skip to main content

TUCTA yalaani taarifa ya upotoshaji ya LHRC yamtaka Mkurugenzi kufuta kauli yake

Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) limemtaka Mkurugenzi wa
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga kufuta kauli yake
kuwa kituo hicho kimebaini vyama vya wafanyakazi havina msaada  na kwamba 
wafanyakazi hufanya kazi kwa muda wa ziada bila malipo pamoja na  kufanya 
bila mikataba ya ajira.

Aidha, TUCTA limesema taarifa hiyo ni upotoshaji na wanaipinga na kwamba 
haina chembe ya ukweli kwani inapingana na takwimu zilizopo kwenye ripoti 
husika.

Hatua hiyo  imekuja hivi karibuni baada ya mkurugenzi  huyo kusikiaka 
akitoa kauli wakati akihojiwa na BBC News akieleza taarifa hiyo iliyoitwa 
ya upotoshaji.

Hayo yamesemwa jijini humo jana na Katibu Mkuu wa  shirikisho hilo,Yahaya
 Msigwa wakati akitoa tamko la kupinga taarifa iliyotolewa na LHRC 
inayoelezea utendaji kazi wa vyama hivyo nchini.

Alisema TUCTA wameisoma ripoti hiyo ya LHRC ya Muhtasari wa Haki za 
Binadamu na Biashara ya mwaka 2017 kwa umakini na kubaini maelezo 
yaliyotolewa yanapingana  kabisa na ripoti ya kituo hicho.

Msigwa amebainisha kuwa vyama vya wafanyakazi  vinafanya kazi kwa misingi 
ya sheria na kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 kama 
ilivyorekebishwa Ibara ya 18 na 19 wamepewa uhuru wa kutoa maoni na 
kujumuika kwa watu wenye masilahi yanayofanana.

Amefafanua kuwa katika ripoti ya LHRC imebainisha kuwa asilimia 74 ya 
wafanyakazi waliohojiwa walisema wana mikabata ya ajira,asilimia 95 
ya wafanyakazi walibainisha wanafanya kazi kwa muda unaotakiwa kisheria,
asilimia 73 wakibainisha mazingira ya kazi ni ya wastani, mazuri na 
mazuri sana.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa asilimia 55 wamepata mafunzo ya afya na usalama
kazini,asilimia 45 walikiri kuwa fidia hutolewa kwa wafanyakazi wanaoumia 
kazini huku asilimia 66 ya wafanyakazi walikiri kuwa na matawi ya vyma hivyo
 huku ripoti hiyo ikiongeza asilimia 90 waliohojiwa walisema wwanakwenda 
likizo kwa muda na kwamba asilimia 75 ya wafanykazi waliotembelewa walisema
 wana utaratibu wa ndani wa kushuhulikia matatizo yao.

Amefafanua kuwa kwenye taarifa hiyo ukurasa wa 13 kuhuusu uelewa wa sheria 
za kazi,haki na wajibu wa wafanyakazi LHRC walikiri wafanyakazi wana uelewa
 wa elimu ya juu ya umuhimu wa vyama hivyo.

Ameongeza kuwa vyama hivyo vinatimiza majukumu yake ipasavyo kwa kuwatetea 
wafanyakazi na kusimamia madai yao.

Kwa upande wake Mwansheria wa TUCTA,Noel Nchimbi amesema matamshi yaliyotolewa 
hayaendani na ukweli ulioko kwenye ripoti ya kituo hicho hivyo kinapaswa kufuta
 matamshi hayo.

Naye Katibu Mkuu wa Tewuta,Junus Ndalo amesisitiza kuwa kituo hicho kimepotea
taarifa ya upotoshaji inavyovishushia hadhi vyama vya wafanyakazi.

Comments