SERIKALI imeridhishwa na mradi wa mapinduzi katika sekta za kilimo na mifugo baada ya mradi huo unaotekelezwa katika halmashauri nne za Mkoa wa Mwanza kuonyesha mafanikio na tija kwa wakulima na wafugaji.
Akizungumza katika mahojiano na waandishi wa habari wilayani Misungwi hivi karibuni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais(TAMISEMI) John Cheyo alisema baada ya kukutana na wakulima walikiri kuwa mradi huo una tija.
“Tulipokutana na wakulima maeneo mbalimbali ya mradi walikiri una tija na hivyo tukiuhamisha na kuupeleka katika mikoa mingine kunaweza kuwa mabadiliko makubwa zaidi kwenye kilimo. Ili kuongeza uzalishaji wakulima wanatakiwa kusaidiwa utaalamu na ushauri wa kupanda mbegu kwa nafasi na matumizi bora ya pembejeo,” alisema Cheyo.
Alifafanua kuwa mradi huo unafanya kazi kwa kushirikiana na serikali ya Mkoa wa Mwanza kwenye maeneo manne kujaribu zao la alizeti huko Buchosa na Sengerema ambako lilikuwa halijaanza ili wawasaidie wakulima walime kibiashara na kuongeza kipato, pia Dalberg inajaribu kuongeza nguvu kwenye zao la pamba liwe na tija zaidi.
Mradi huo pia unawajengea uwezo maofisa ugani na mifugo kwa kuwapa kompyuta, vifaa vya kazi na usafiri ili kufuatilia na kukusanya taarifa, kutunza takwimu na kumbukumbu kwa kutumia kompyuta.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi Dalberg Tanzania Steve Kisakye alisema kuwa mwaka 2016 serikali kupitia sekta ya kilimo na mifugo ilianza kufanya kazi na Dalberg 3D ikijikita kwa kutoa mafunzo na ufadhili wenye tija kwenye kilimo na ufugaji katika kuongeza uwezo kwenye sekta hiyo.
Alisema mradi huo unaotekelezwa katika halmashauri za Misungwi, Kwimba,Sengerema na Buchosa mkoani Mwanza unalenga kuibua mbinu mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za kilimo na ufugaji kwa kuzingatia vipaumbele vya kila halmashauri.
Kisakye alieleza kuwa mradi wa Dalberg 3D wa kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo uliombwa na kubuniwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) ili kuangalia mabadiliko yanayotakiwa licha ya wengi kuchangia hakukuwa na mchango wa kuisadia serikali iendele mbele na kuleta mabadiliko kwa wakulima na wafugaji.
“Serikali inafanya kazi kubwa ya kuwasaidia maofisa ugani kwa kuwajengea uwezo na kuwawezesha wakulima kupanga mikakati mipya ila hakukuwa na mchango wa kuisaidia serikali kuleta mabadiliko chanya ili iweze kwenda mbele.Hivyo mtizamo wa serikali ni kwamba hakukuwa na usaidizi wa kuisadia taaluma ya masuala ya ugani,”alisema Kisakye.
Aliongeza kazi kubwa ya mradi wa Dalberg 3D ni kuwajengea uwezo na kuwapa taaluma mpya, kupanga mipango kabambe na mikakati mipya katika kuendeleza tija kwenye kilimo na ufugaji,ukusanyaji wa taarifa na kuzichambua ili zifanyiwe kazi.
Wakizungumza kwa nyakati maofisa kilimo na ugani wa halmashauri za Misungwi, Sengerema na Kwimba walisema yapo mabadiliko makubwa kwa wakulima baada ya kupata elimu na matumizi bora ya pembejeo.
“Mradi huu umebadili mitizamo ya watumishi wa umma katika sekta hizi (kilimo na mifugo) kwa kila mmoja kujua wajibu wa kufanya kazi si lazima afundishwe,”alisema Afisa Kilimo Kwimba Alfred Mabuga.
Naye Afisa Kilimo Wilaya ya Misungwi Kwilasa Mahigu alisema “ Matarajio ni kuongeza tija ili ekari moja ya pamba iliyokuwa ikizalisha kilo 250 hadi 300 izalishe kilo 700 hadi 850. Hivyo ufanisi umepatikana baada ya Dalberg kuwasaidia maofisa wetu kufikisha mbegu bora na kwa wakati katika kata na vijiji, kufuatilia na kutoa mbinu bora kwa wakulima.”
Aidha, mmoja wa wakulima wa wilayani Sengerema Ndaki Butulya kwa niaba ya wenzake alisema mashamba yao walikuwa hawayatunzi kitaalamu lakini baada ya kupata elimu na kuanza kutumia mbolea ya kupandia na kukuzia mazao baada ya palizi sasa wanapata mavuno mengi.
Baadhi ya wakulima wilayani Sengerema wakiwa katika moja ya shamba darasa la zao la pamba walilolianzisha baada ya kupata elimu kwa ufadhili wa mradi wa Dalberg 3D.
Afisa Mfugo Wilaya ya Misungwi Dk. Chrispine Shami (mbele), Mratibu wa Dalberg wilayani humo Ines Muganyizi wakimuongoza Mkurugenzi wa Uratibu (TAMISEMI)Dk. Andrew Komba (wa tatu nyuma)kukagua mashamba ya mfano ya utekelezaji wa mradi wa Dalberg 3D wilayani humo.
Mfugaji wilayani Misungwi ambaye jina lake halikupatikana mara akiswaga ng’ombe wake kuingia ndani ya josho kwa ajili ya kuwaogesha dawa ya kuua wadudu. Josho hilo ni moja kati ya majosho yaliyofufuliwa kwa ufadhili wa mradi wa Dalberg 3D unaotekelezwa katika halmashauri nane za Mkoa wa Mwanza ambapo wameanza kuzingatia elimu ya ufugaji wanayopewa na wataalamu wa mifugo kupitia mradi huo.
Mkurugenzi wa mradi wa Dalberg Tanzania Steve Kisakye (kushoto) akitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais(TAMISEMI) John Cheyo (katikati)kabla ya kukabidhi pikipiki za usafiri kwa maofisa ugani na mifugo katika Wilaya ya Sengerema.Kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Alfred Kipole.
Mkurugenzi wa Dalberg Steve Kisakye (kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais (TAMISEMI) John Cheyo pikipiki kwa ajili ya usafiri wa maofisa Kilimo (ugani) na Mifugo katika Wilaya ya Sengerema ili ziwarahisishie usafiri wa kwenda vijijini kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji pamoja na kukusanya taarifa.
Mkurugenzi wa Uratibu (TAMISEMI) Dk. Andrew Komba (mwenye shati la drafti) akimsikiliza ofisa Ugani wa Kata ya Mondo katika wilaya ya Misungwi John Choto baada ya kukagua shamba la pamba la mkulima Muhoja Ngole (kushoto). Mkulima huyo amelima na kulitunza shamba hilo kwa kuzingatia ushauri wa watalaamu chini ya ufadhili wa Mradi wa Dalberg.
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps
Comments