Askari jeshi zaidi ya 800 wakiwemo baadhi ya maafisa wakuu katika jeshi la Rwanda wamestaafishwa.
Miongoni mwa waliostaafishwa ni majenerali wawili waliowahi kuongoza idara za upelelezi za nchi hiyo, Jenerali Karenzi Karake na Jenerali Jack Nziza.
Mwaka uliopita majenerali hao walibadilishiwa nyadhifa walizokuwa nazo jeshini, hatua ambayo kwa baadhi waliifasiri kuwa kama kushushwa ngazi.
Kulingana na wizara ya ulinzi ya Rwanda baadhi ya waliostaafishwa wamekamilisha mikataba yao jeshini na wengine ni kutokana na sababu za ugonjwa.
Mwandishi wa BBC aliyepo Kigali Yves Bucyana anasema kwa jumla maafisa waliostaafishwa ni 817.
Luteni jenerali Karenzi Karake kwa muda mrefu aliongoza idara ya upelelezi ya Rwanda na nje ya mipaka ya nchi hii akawa naibu kamanda wa kikosi cha umoja wa mataifa cha kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan.
Naye Brigedia jenerali Jacques Nziza alishika nyadhifa mbali mbali katika wizara ya ulinzi ukiwemo wadhifa wa mkuu wa vitengo vya upelelezi.
- Kagame abadilisha baraza la mawaziri Rwanda
- Vyama vikongwe vyamtangaza kagame kuwa mgombea Urais Rwanda
- Rwanda yawafuta kazi polisi 200 wafisadi
Mwaka 2015 akiwa mkuu wa upelelezi, jenerali Karenzi alikamatwa mjini London kufuatia waranti ya kimataifa iliyotolewa na nchi ya Uhispania ikimhusisha yeye na maafisa wengine wa jeshi la Rwanda kwa makosa ya uhalifu wa kivita nchini Rwanda na jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Hata hivyo, baada ya pilka pilka za kidiplomasia Uingereza ilimwachia huru kwa kile ambachoJaji alisema sheria za nchi hizo mbili hazilingani.
Pamoja na hayo, mageuzi ya mwaka uliopita ndani ya jeshi ambapo majenerali hao walibadilishiwa nyadhifa, kwa baadhi yalitafsiriwa kama kushushwa ngazi.
Jenerali Karenzi aliachishwa kazi ya mkuu wa upelelezi na kutangazwa kama mshauri wa rais wa masuala ya kijeshi huku Jacques Nziza akapewa wadhifa wa kuongoza kitengo cha kuratibu shughuli za jeshi na wananchi.
Tangazo la wizara ya ulinzi ya Rwanda, pamoja na kuonyesha picha za karamu iliyoandaliwa kwa ajili ya waliostaafishwa, limeelezea tu kwamba miongoni mwa askari hao, zaidi ya 300 walikuwa mchanganyiko wa maafisa wakuu na maafisa wa dogo, na kwamba baadhi walihitimisha mikataba yao na jeshi la RDF huku wengine 70 wakistaafishwa kwa sababu ya ugonjwa.Source BBC.
Comments