Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) Amina Makilagi amesema wanaunga mkono tamko la Rais Magufuli kwamba, ni marufuku kwa msichana aliyepata ujauzito kuendelea na shule kwa sababu ni maelekezo yaliyomo katika ilani ya Uchaguzi 2015-2020.
Makilangi amesema, UWT inaunga mkono tamko hilo kwa kuwa Sera ya Serikali ni kusimamia utoaji wa elimu katika mfumo rasmi nchini na kwamba kwa wale watakaokatisha masomo basi njia mbadala za kusoma ndizo zinazofaa kutumika.
"Tafiti mbalimbali za Jumuia na Taasisi nyingine hapa nchini na za Kimataifa likiwemo Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataida (UNICEF), Mwanafunzi mjamzito au aliyejifungua ni vigumu kuendelea na masomo katika mfumo ambao umeandaliwa kulingana na Saikolojia ya akili ya mtoto asiye na majukumu ya malezi na ndiyo maana upo mfumo uliopendekezwa na sera na ilani ya CCM kwamba anayekatiza masomo katika mfumo rasmi anaweza kuendelea katika mfumo usio rasmi, Mifumo isyo rasmi kwa ajili ya wanafunzi wa aina hiyo na wengine waliokosa masomo katika mfumo wa kawaida ni kama MEMKWA na QT" , alisema Makilagi.
Alisema UWT inatambua na kuheshimu mapendekezo ya tafiti hizo kuhusu watoto na pia inakubaliana na sera ya Serikali na Ilani ya CCM kuweka utaratibu bora na wenye manufaa zaidi wa kuwazuia wajawazito na wazazi kuendelea na masomo katika mfumo rasmi na badala yake kutengeneza mfumo mbadala wa kupata elimu kwa kuwa kufanya hivyo kumaimarisha nidhamu, na uwezo wa kitaaluma wa watoto.
"Pia UWT inawapongeza Wabunge kwa kupitisha sheria kali kwa wale watakaobainika kusababisha upatikanaji wamimba kwa wanafunzi, kutetea na kufanikisha ndo za utotoni. Sheria ya maraekebisho ya sheria mbalimbali namba 2 ya mwaka 2016 ilyofanyiwa marekebisho ya sheria ya elimu ya Sura 353 inaweka wazi dhamira ya Serikali ya kumlinda mtoto wa kike na kutoa onyo kali kwa wale wenye tabia za kuwarubuni na kuwasababishaia mimba zisizotarajiwa na za utotoni", aliongeza.
Pamoja nakuunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais, UWT imewashauri na kuwaomba wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, kuwalinda watoto wa kike na kutoa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya jinsia, athari za mimba za utotoni na athari za maambukizi ya magonjwa ya zinaa ukiwemo Ukimwi.
Comments