Na Salym Juma, Arusha
Nikinukuu kauli ya Abdi Banda katika maandishi kwamba, wachezaji
wajitume na wanatakiwa kuwa makini na nafasi, hasa zinapotokea nafasi za
kutoka kwenda kucheza nje ya nchi na wasiangalie nyuma. Kauli ya Beki
huyu wa zamani wa Simba inawagusa Wachezaji ambao wanaamini Simba na
Yanga ndio sehemu pekee ya mafanikio ambayo wanapaswa kufika. Ukweli ni
kwamba hata hao akina Samatta na Ulimwengu walifika hapo walipo baada ya
kuondoka Tanzania na kwenda kujaribu bahati zao nje.
Kufanya vizuri kwa Abdi Banda msimu uliopita kumemfanya mchezaji huyu
kupata nafasi ya kusajiliwa na timu iliyoshiriki ligi kuu ya South
Afrika msimu uliomalizika. Banda ambaye tayari alishasaini mkataba wa
kujiunga na klabu hiyo wakati akiwa kwenye michuano ya COSAFA Cup 2017
iliyofanyika South Afrika anakwenda kucheza kwenye ardhi ya Mandela na
kama akikitumia vyema kipaji chake huenda akapata shavu kwenye vilabu
vikubwa vya South Afrika.
Banda ni aina ya wachezaji ambao hupenda sana kuuchezea mpira na mara
nyingi hujaribu kupiga mashuti ya mbali langoni mwa mpinzani. Kitu cha
msingi cha kuzingatia ni nidhamu kwani wachezaji wetu wanapaswa kuiga
nidhamu ya akina Samatta au Himid Mao. Japo Banda amekuwa na nidhamu
yenye mashaka na makosa ya hapa na pale ila naamini anao muda mzuri wa
kurekebisha haya kabla ya kuanza kukipiga klabuni.
Watanzania wengi wanatamani kuijua kwa undani timu hii anayokwenda mchezaji huyu wa zamani wa Simba na Taifa Stars kwa sasa.
Baroka F.C ni klabu iliyopo South African inayotokea Ga-Mphahlele
karibu na Polokwane, Limpopo. Timu hii ni miongoni mwa timu
zilizoanzishwa hivi karibuni na imekuwa na mwenendo wa kuridhisha kadiri
siku zinavyosonga. Tangu mwaka 2007 ilipoanzishwa ilijitahidi kupanda
daraja kwenye msimu wake wa kwanza ila mechi ya mwisho kabisa
iliwakwamisha baada ya kutoka sare na Thanda Royal Zulu. Baroka ni Timu
changa ambayo inaweza kuwa na uhai mrefu huko tunapoelekea.
Comments