SERIKALI ya Norway imeipatia Tanzania msaada wa Dola Milioni 10 za Marekani kupitia programu ya maboresho ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, inayotarajiwa kuanza Mwaka Mpya wa Fedha- Julai Mosi mwaka huu.
Mpango huo pamoja na uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Mafuta, umezinduliwa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Borge Brende, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana Pallangyo kwa niaba ya Serikali zao.
Dkt. Mpango ameishukuru Serikali ya Norway kwa msaada huo mkubwa utakaochangia kuboresha utendajikazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuijengea uwezo zaidi wa kitaalamu, miundombinu na vitendeakazi vingine vitakavyo changia kuongeza uwezo wa Mamlaka hiyo wa kukusanya mapato ya Serikali.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana Pallangyo amesema kuwa hatua ya Serikali ya Norway kuendelea kufadhili programu ya pili ya Mpango wa kuendeleza Sekta ya Mafuta utaiwezesha Serikali kubobea katika masuala ya utaalamu wa masuala ya sheria na usimamizi wa sekta hiyo.
Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Borge Brende amesifu utendaji kazi mahili wa Mhe. Rais Dokta John Pombe Magufuli wa kupambana na ufisadi na vitendo vya rushwa pamoja na kuimarisha ukusanyaji kodi, hatua ambayo itaifanya nchi ipige hatua za maendeleo haraka.
Amesema kuwa hajawahi kuona nchi yoyote duniani ikiendelea bila kuweka nidhamu na uwajibikaji serikali pamoja na kutokusanya mapato yake ipasavyo na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya tano kufanikisha mipango yake ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Comments