Kikosi cha timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’,
kinatarajiwa kwenda Kigali, Rwanda kesho Jumatano mchana kikitokea
Mwanza, Tanzania.
Taifa Stars iliyokuwa jijini Mwanza kwa kambi kabla ya kucheza mchezo
wa kwanza dhidi ya Rwanda Jumamosi iliyopita, itapitia Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere kwenda Rwanda.
Stars itaondoka Mwanza kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania
majira ya saa nne asubuhi na kuwasili Dar es Salaam majira ya saa sita
mchana kabla ya kuunganisha ndege ya Rwanda majira ya saa nane alasiri
kwenda Kigali, Rwanda.
Inakwenda Kigali kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Rwanda maarufu
kama Amavubi kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa
wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN 2018). Fainali za CHAN mwakani
zitafanyika nchini Kenya.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza
timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Mshindi wa jumla katika michezo
miwili, atakuwa amesonga mbele hivyo kukutana na Uganda mwezi ujao.
Katika mchezo huo wa marudiano utakachezwa Kigali Rwanda, Kocha Mkuu
wa Taifa Stars, Salum Mayanga atamkosa beki wake wa kulia, Shomari
Kapombe anayesumbuliwa na mguu alioumia katika mchezo kwanza.
Comments